TAHARIRI: Mawaziri wamulike zaidi maafisa wa KNEC
NA MHARIRI
KWA mara nyingine, ushirikiano wa karibu uliopo kati ya Wizara za Elimu na Usalama wa Ndani na Baraza la Mitihani ya Kitaifa nchini (KNEC) katika maandalizi ya mitihani ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) ni hatua nzuri ambayo itasaidia kukomesha visa vya wizi wa mitihani ambavyo vilikuwa vimeongezeka pakubwa nchini.
Kwa mara ya kwanza, Wakenya sasa wameanza kuwa na imani na vyeti vinavyotolewa na KNEC wakijua kwamba, alama kwenye vyeti hivyo inasheheni uwezo na maarifa sambamba ya mtahiniwa.
Ni jambo la kutia moyo kwamba, Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akifuatilia kwa karibu maandalizi hayo na kutoa onyo kali kwa magenge ambayo yamegeuza mitihani hiyo kuwa kitega uchumi.
Kwa miaka mingi, magenge hayo yamekuwa yakishirikiana na maafisa laghai katika KNEC kusambaza mitihani ya kitaifa mapema kabla ya wakati wake.
Mazingira ya sasa bila shaka yatawatuza wanafunzi wanaotia bidii masomoni na kuwanyima wale wanaotumia fedha kujipatia nafasi ya kujiunga na vyuo taasisi za elimu ya juu.
Isitoshe, hatua hii itakomesha hali ambapo wanafunzi wanazoa alama za juu na kuteuliwa kusomea kozi kama vile udaktari na uhandisi kisha wanalazimika kuzitelekeza ama kutimuliwa kabisa kutokana na ufahamu wao mdogo.
Na katika hali ambapo baadhi wamenusurika kutemwa, matokeo ni kwamba, kumekuwa na wahandisi na madaktari ambao hawakufinyangwa wakaiva vyema.
Wanapoajiriwa, wanaonyesha utepetevu mkubwa pamoja na kushindwa kutekeleza majukumu ya kimsingi mahali pao pa kazi.
Tunaunga mkono matamshi ya mwenyekiti wa KNEC Prof George Magoha kwamba, wakati wa wanafunzi kupata alama ‘A’ za kishenzi umewadia. Kila mwalimu na mzazi ahakikishe wanafunzi wao wamepewa mazingira bora ya kujinoa ili kukabiliana na maswali darasani bila usaidizi wa aina yoyote kwa njia ya udanganyifu.
Sekta ya elimu imepanuka pakubwa katika muda wa miaka 15 iliyopita, hasa kutokana na sera ya elimu msingi bila malipo iliyoanzishwa na Rais mstaafu Mwai Kibaki.
Serikali ya sasa imewezeka zaidi katika sekta hiyo kiasi kwamba, sehemu kubwa ya bajeti ya kitaifa inatengewa elimu. Juhudi hizo zote hazipaswi kuruhusiwa kuhujumiwa na walaghai wanaotaka kuvuna wasikopanda.
Na kwa maelfu ya watahiniwa ambao wanajiandaa kufanya mitihani yao ya darasa la nane na kidato cha nne, bila shaka ushauri wetu ni huu: Njia za mkato zina miiba mingi na mara nyingi hazizalishi matunda. Jiandae kikamilifu na ushindi utakuwa ni wetu. Kila la kheri.