Makala

TAHARIRI: Ukatili wa polisi dhidi ya waandishi ulikiuka haki

April 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

UKATILI uliotekelezwa na maafisa wa polisi dhidi ya wanahabari katika Uwanja wa Ndege wa JKIAmnamo Jumatatu wakati wa kurejea nyumbani kwa wakili Miguna Miguna unafaa kukemewa vikali.

Shambulizi dhidi ya wanahabari halikufaa kwa kuwa walikuwa wakiwahudumia Wakenya waliokuwa wakifuatilia taarifa hiyo kwa hamu na ghamu.

Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet anafaa kuhakikisha maafisa waliohusika wanakabiliwa kisheria kwa udhalimu waliotendewa wanahabari hao.

Wanahabari hawafai kukabiliwa kama majangili wanapotekeleza kazi yao ya kupasha umma, haswa katika nchi inayojigamba kuwa inakumbatia mfumo wa utawala wa sheria.

Uhuru wa wanahabari umenakiliwa vizuri katika Katiba iwapo, kwa vyovyote vile, polisi na serikali kwa jumla, wamesahau hilo.

Kwa kweli idara ya polisi imegeuka kwa mkiukaji mkuu wa sheria na inayofanya mambo itakavyo. Marejeo ya Dkt Miguna na visanga vilivyogubika kurejea kwake vilikuwa habari ambazo Wakenya walifuatilia kwa makini sana.

Ni vizuri kutambua kwamba hakuna sheria inayowazuia wanahabari kuripoti visa vinavyotokea katika uwanja wa ndege, kwa hivyo ukatili wa polisi haukuwa na msingi wowote.

Polisi wana tabia ya kupuuza sheria na hili lilifahamika wazi baada ya kulaumiwa na Mashirika ya Kutetea Haki za Kibinadamu kwa mauaji ya waandamanaji mwaka jana.

Wakati huo, polisi walitumia nguvu kupita kiasi kuwakabili viongozi na wafuasi wa upinzani na hata watoto wadogo wasiojua chochote kuhusu siasa kama ‘Baby Pendo’.

Kenya siyo taifa linaloongozwa na polisi bali katiba na sheria. Hivyo basi, polisi walifaa kufahamu hilo kabla ya kutekeleza unyama wao.

Yaliyojiri katika uwanja wa JKIA yalisawiri nchi yetu vibaya machoni pa mataifa ya nje, haswa kuhusu uhuru na haki za wanahabari na raia wa taifa letu.

Uwanja huo uligeuzwa jukwaa la kivita kwa sababu ya mambo mepesi ambapo njia bora ingetumika hali ingekuwa shwari.

Ili kuonyesha mfano bora, Bw Boinnet anafaa kuwakabili polisi hao na kuhakikisha wamekamatwa na kushtakiwa mahakamani.

Iwapo kila mara polisi wataruhusiwa kutenda maovu na hawachukuliwi hatua, basi tutarajie mabaya zaidi siku za usoni.

Wakenya wana haki ya kupata habari,jukumu ambalo wanahabari wanapaswa kulitekeleza bila vitisho kutoka kwa polisi.