Makala

Tilapia wa bei nafuu kutoka Uchina ni hatari kwa afya – Utafiti

December 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 3

Na ALLAN OLINGO na FAUSTINE NGILA

UTADHANI kitoweo cha samaki unachokula kwenye mikahawa ya mijini hapa Kenya kimetoka kwa maziwa ya humu nchini lakini ukweli ni kwamba kimeagizwa kutoka Uchina huku asasi husika ya udhibiti wa ubora wa bidhaa ikionekana kulemewa na kazi yake.

Hii ni kulingana na uchunguzi kwenye maabara uliofanywa na shirika la habari la Nation Media Group (NMG) mwanzoni mwa Desemba mwaka huu.

Katika soko la Gikomba, Nairobi, samaki kutoka Uchina huuzwa hadharani baada ya kutolewa kwa maboksi na kupakiwa upya kwa vikapu na wafanyabiashara wa humu nchini.

Mchakato huu huhusisha kutoa samaki waliohifadhiwa kwa maboksi ya friji, ambayo huwa wamewekewa muda wa matumizi wa miaka miwili, na kuwaweka kwa mifuko na kusambazwa katika maeneo mbalimbali ya jiji kwa mikokoteni.

Iwapo utauliza walikovuliwa samaki hao, jibu ni moja – Ziwa Victoria. Lakini uchunguzi wa maabara wa NMG umefichua kuwa samaki hawa kutoka Uchina wamejaa chembechembe za madini ya zebaki, copper, lead na vyuma vya risasi hali inayohatarisha maisha ya mamilioni ya Wakenya.

Hata hivyo, shirika la Udhibiti wa Ubora wa Bidhaa nchini (KEBS) limekana matokeo ya uchunguzi huo, likisema samaki hao hawana madhara yoyote kwa afya ya wanadamu.

KEBS ilisema kuwa uchunguzi wa samaki kutoka maeneo mbalimbali katika maabara yake haukupata chembechembe hizo.

“Bidhaa zote zinazoagizwa kutoka mataifa ya nje zinatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa ubora katika taifa zinakotolewa, na zinapotimiza viwango vya ubora, hukabidhiwa cheti cha ubora. Zikifika hapa Kenya, bidhaa hizo huchunguzwa tena,” likasema shirika hilo.

Lakini bidhaa hizo zinapotua hapa nchini, hazifanyiwi uchunguzi wa maabara na hivyo kuwaacha walaji wa samaki katika hatari ya bidhaa zilizoidhinishwa na Uchina.

Samaki hawa wa Uchina huvutia wafanyabiashara wengi kwa kutoka na bei yake nafuu maanake boksi lenye samaki 60 huuzwa kwa Sh2,700 huku samaki mmoja kutoka Ziwa Victoria akiuzwa kwa Sh450.

Kitoweo cha samaki kimekuwa maarufu sana katika mikahawa, masoko ya mitaani, kwenye vioski, kwenye magenge ya chakula kando ya barabara na katika soko kuu la Gikomba kutokana na bei ya chini huku samaki wanaofugwa humu nchini wakikosa kutimiza hitaji la soko.

Wakati NMG ilipeleka sampuli za samaki kutoka Uchina iliyonunua katika soko la Gikomba, kwa maabara ya Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN), ilipata chembechembe za lead, copper, mercury na arsenic kwa sampuli hizo.

Matokeo yalionyesha chembechembe 0.04 ppm (vijisehemu katika kila milioni) za lead, 0.005 ppm za mercury, zaidi ya 0.001 ppm za arsenic na 1.2 ppm za copper na kuthibitisha uwepo wa madini hayo katika maji ambamo samaki hao wanafugiwa.

“Ulaji wa muda mrefu wa samaki hawa unaweza kuwaletea walaji madhara mengi mwilini,” akasema Prof James Mbaria, mkuu wa idara ya Afya ya Umma katika UoN.

Uwepo wa vyuma hivi katika samaki hawa unamaanisha samaki hao wamefugwa katika mazingira ambapo mafuta ya petroli hutumiwa kwa pampu ya maji au kifaa cha kunyunyizia dawa za kuua wadudu na magonjwa na kupelekea chembechembe zake kuingia majini.

NMG ilifanya uchunguzi huo kufuatia hofu ya kiafya kutokana na samaki wa Uchina, hasa Amerika, iliyoitaka Uchina izingatie zaidi sheria za uuzaji wa samaki kimataifa.

Uchunguzi huo wa maabara ulilenga kung’amua kiwango cha dawa za kuua wadudu zikiwemo streptomycin, sulfadimidine, oxytetracycline, na penicillin.

Matokeo ya uchunguzi huo hayakuonyesha uwepo wa dawa yoyote kwenye sampuli hizo.

Katika miaka ya hivi majuzi, Kenya imegeukia soko la Uchina kutosheleza hitaji lake la samaki, na kupelekea kuongezeka maradufu kwa kiwango cha samaki inachoagiza kutoka taifa hilo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kutoka thamani ya Sh1.1 bilioni hapo 2016 na kufikia 2.1 bilioni 2017.

Hii imeibua maswali kuhusu mtindo wa taifa hilo la bara Asia kujaza soko la samaki la Kenya wavuvi na wafugaji wa samaki wa humu nchini wasipate pa kuuza samaki wao.

Kulingana na takwimu za Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS), Kenya ilitumia Sh2.2 bilioni kununua samaki katika miezi ya kwanza 11 ya 2017, ishara ya jinsi Uchina inadhibiti soko la samaki humu nchini – zaidi ya asilimia 90.

Mauzo ya samaki ya Uchini humu nchini ambayo yalikuwa Sh620 milioni hapo 2015, yanajiri wakati uzalishaji wa samaki umedidimia katika maziwa ya Kenya.

Samaki wa friji pamoja na tilapia waliongoza katika uagizaji kutoka Uchina, wakiwa tani 18,000 wa thamani ya Sh1.8 milioni.

Lakini si samaki wa kuagiza kutoka nje pekee wana chembechembe za vyuma. Utafiti uliofanywa na mashirika kadha umeonyesha kuwa samaki wanaofugwa humu nchini pia wana chembechembe hizo.

Miaka miwili iliyopita, utafiti uliofanya na UoN ulioongozwa na Dkt Isaac Omwenga ulipima sampuli 213 za samaki kutoka vidimbwi 60 vya samaki katika kaunti za Kiambu na Machakos na kupata zimejaa dawa za kilimo zilizopigwa marufuku, zinazosababisha saratani.

Idara ya Afya ya Umma ya UoN hapo Juni 2013 ilipima sampuli za samaki na mchanga wa Kirinyaga na kupata viwango vya juu vya madini ya lead, ambavyo ilisema vilitokana na mbinu za kilimo katika kaunti hiyo.

“Vyuma vinavyoweza kupatikana ndani ya samaki ni mercury, cadmium, arsenic, chromium, thallium na lead ambavyo huingia katika mzunguko wa chakula na kuwadhuru wanadamu hata katika viwango vya chini.”

“Ukila samaki hao, chembechembe hizo husafirishwa kwa mfumo wa damu hadi kwa ini au mifupa ambapo zinahifadhiwa,” wakasema watafiti hao kwenye ripoti waliyochapisha katika kijitabu cha Sayansi na Usafi wa Mazingira.