Makala

UMBEA: Usiingie uhusiano sababu ya tamaa ya fedha au mwili

January 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SIZARINA HAMISI

PITAPITA zangu wakati mwaka huu unapoanza, nimebaini wengi walio kwenye ndoa ama uhusiano, wanaishi kwa mazoea.

Na sio kwa upendo, maelewano na mtizamo wa pamoja.

Wengi niliozungumza nao hawakuficha kwamba wamekinai uhusiano, ndoa ama mapenzi na wenzao na kuwa kwao pamoja ni pengine kuamua kuishi kwa uvumilivu ama kusukuma siku, bora zisonge.

Wengine wakanieleza kwamba wameendelea kuwepo kwenye uhusiano ama ndoa sababu hawajaona mbadala wa hatua ya kuchukua.

Mtu yupo na mwenzake ilimradi tu kwa sababu yupo na hana namna nyingine. Hamjali mwenzake, hana tena hisia naye, kilichobaki ni zile hadithi za kuwahadithia wenzake kwamba na mimi nina mke au mume. Mimi nipo kwenye uhusiano na fulani.

Shida hii inawatesa sana walioko kwenye ndoa. Kwa uzoefu nilionao, kupitia maoni ninayoyapata kutoka kwa wasomaji na mazungumzo yangu na watu mbalimbali, ninapata picha kwamba mambo sasa hivi kwenye uhusiano yanakwenda kombo.

Kwani imekuwa kawaida mwanaume kukosa hamu na mkewe na mke naye ni hivyo, hana hamu na mumewe. Hii ndiyo tunasema watu wamechokana, watu wamekinai. Yale mapenzi waliyokuwa wanapeana wakati wanaanza uhusiano au miaka miwili mitatu ya awali, si ya sasa.

Inafika mahali, mke anakwambia amechoka hivyo anaona ni bora kuanzisha uhusiano usio rasmi ilimradi tu kupata furaha ya moyo. Anaamini kwamba akiwa na mpango wa kando atakuwa na furaha zaidi na kuondoa kero zilizopo kwenye ndoa na mumewe.

Yuko radhi aopoe kijana mbichi amgharimie mahitaji yote muhimu ili ampe hitaji la moyo wake. Mara nyingi ukichunguza kwa undani, si kwamba mume wake hawezi kumtimizia mahitaji, anaweza tena kupitiliza, isipokuwa yale mazoea na kuchukuliana poa ndio yanawatafuna.

Mume naye anamchukulia poa mkewe, anatafuta msichana mbichi huko nje, anaamua raha na starehe yake atakuwa anaipata huko nje. Nyumbani watakutana jioni, kila mmoja anafanya mambo yake kwa siri na anajiona mjanja kwamba mwenzake hajui.

Mwisho wa siku wote wanakuwa wanaishi tu ilimradi maisha yaendelee. Upendo ndani ya nyumba unakuwa haupo tena. Inapofikia hatua hii, ni wazi uhusiano ama ndoa inaelekea kusambaratika kimya kimya ama kwa dhoruba. Kwani kuishi na mke au mume kwa mazoea ya aina hii ni sawa na kuishi na nduguyo ambaye unamheshimu lakini huwezi kumgusa.

Itafika mahali maana halisi ya ninyi kuwa wanandoa inakuwa haipo. Hivyo basi, ni vyema kupata elimu juu ya hili ili kama imekutokea au haijakutokea bado, ujue namna ya kujihadhari na shida hii ambayo inawatafuna wengi.

Shida hii husababishwa na mengi, yawezekana ikawa ni mabadiliko ya tabia, yawezekana ikawa pia ni hulka au utashi wa mtu. Yawezekana ikawa ni mapenzi ambayo tangu awali hakuwa nayo kwako. Mtindo huu wa uhusiano una changamoto.

Kitendo cha mtu kuingia kwenye uhusiano nawe halafu hakupendi kwa dhati, ni shida. Matokeo yake yanagharimu maisha yenu yote ya ndoa ama uhusiano. Kama ni mabadiliko ya tabia, ni suala la kujitathmini na kuona kwamba unafanya makosa, hivyo rudisha thamani kwa mke au mumeo.

Kama ni suala la tabia, basi badilika. Rekebisha tabia ambayo inahatarisha uhusiano wenu. Cha muhimu zaidi, kama ndiyo kwanza unaingia kwenye uhusiano, basi hakikisha unaingia na mtu ambaye kweli unampenda kutoka moyoni.

Usiingie kwenye uhusiano na mtu kwa tamaa ya fedha au mwili. Ishi na mtu ambaye kweli utampenda na hata ikitokea siku umeanguka, basi rudi kwenye mstari na umuheshimu mtu wako.

Ukiwa umefikia hatua ya kukinai, jiulize uliyenaye ni mtu uliyempenda tangu zamani? Kama jibu ni ndiyo, jiulize ni kwa nini ukinai sasa? Tafakari na uchukue hatua mwaka huu unapoanza.

 

[email protected]