Makala

Uteuzi wa Kindiki unavyopasua Mlima Kenya

Na LABAAN SHABAAN October 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BAADA ya wabunge na maseneta kumfukuza kazi aliyekuwa Naibu wa Rais, Rigathi Gachagua sasa huenda amepata marafiki wapya, ikidhihirika wazi kuwa waliokuwa wandani wake wakiongozwa na Rais Ruto hawataki kumuona.

Tayari Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki ameteuliwa na kuidhinishwa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Bw Gachagua.

Alhamisi katika kikao cha mjadala wa kumbandua Naibu wa Rais Gachagua, wakili wake mkuu Paul Muite pamoja na uongozi wa hospitali ya Karen walitangaza kuwa Bw Gachagua alikuwa amelemewa na maradhi ghafla na baadhi ya wabunge wakaelekea moja kwa moja hadi katika hopitali ya Karen, wengine hisia zikawapanda.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Kinara wa Chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa, Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba, Seneta wa Kitui Enoch Wambua na aliyekuwa Mbunge wa Kaunti ya Laikipia walimtembelea hospitalini Karen.

Kuna ishara kwamba huenda kukawa na muungano mpya wa kisasa ambao utamhusisha Rigathi Gachagua na Kalonzo Musyoka pamoja na Kiongozi wa DAP – K Eugene Wamalwa, ambao sasa huenda ukawa mwiba mpya kwa Rais William Ruto na Raila Odinga.

Isitoshe, maseneta wa chama cha Wiper hawakuunga mkono kubanduliwa kwa Gachagua.

Iwapo muungano huo utakamilika basi, Rais William Ruto atakuwa na kizingiti kipya cha kisiasa kuzingatia.

Mnamo Oktoba 14, Bw Musyoka, alikosoa mchakato wa kumfurusha Naibu Rais Rigathi Gachagua akisema wabunge wa Wiper waliounga hoja hiyo wataadhibiwa.

Bw Musyoka aliwakosoa wabunge 282 waliounga mkono mswada huo uliowasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse.

Alisema wale wa Wiper ambao waliunga hoja hiyo lazima wafike mbele ya kamati ya nidhamu chamani na kueleza kwa nini walikiuka maagizo ya kutounga hoja hiyo.

“Serikali kwa hakika imeshika mateka bunge. Kama hilo halikuwa wazi hapo mbeleni, matukio ya kutimuliwa kwa Bw Gachagua yalithibitisha. Wabunge wa Wiper waliounga hoja hiyo wajiandae kukabiliwa na adhabu ya chama,” akasema.

Makamu huyo wa rais wa zamani aliandamana na kiongozi wa chama Democratic Action Party-Kenya, Eugene Wamalwa, Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, Gavana wa zamani wa Kiambu na wanasiasa kadhaa wa Wiper kule Mlolongo alipoyatoa madai hayo.

Bw Musyoka alisema kuwa hana imani na wabunge na maseneta, korti ni kati za asasi ambazo zimetekwa na serikali.

Pia alimhusisha Kinara wa Azimio Raila Odinga kwenye mikataba ya mabilioni ya pesa baina ya serikali na shirika la India.

Alisema mikataba hiyo inayohusu sekta za nishati, huduma ya afya na usafiri, ni kiumbe cha serikali pana inayojumuisha serikali ya Kenya Kwanza na wandani wa Bw Odinga.

Matamshi ya Bw Musyoka yamejiri huku Waziri wa Nishati, Opiyo Wandayi, mwandani wa Bw Odinga akifichua kuwa serikali ilitia saini mkataba wa Sh95 bilioni na Adani Energy Solutions kuimarisha usambazaji wa umeme.

Kampuni hiyo ya India inashiriki mazungumzo na serikali kuhusu kuboresha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Inasemekana kuwa kampuni hiyo ya India imetia saini mkataba na serikali kuendesha ajenda ya mpango wa afya kwa wote.