Wavuvi Wakenya wasimulia walivyoteseka gerezani Madagascar
MIEZI minne iliyopita, wavuvi watatu waliondoka nchini Kenya wakiwa katika meli ya humu nchini kwa jina “Maab Aqua” bila kufahamu kuwa ndio ulikuwa mwanzo wa masaibu katika nchi ya kigeni.
Mabw Mbarak Awadh Mbarak, Mohamed Bakari, na Karisa Gona Nguma ambao walikamatwa mnamo Julai 2024, kwa madai ya kujihusisha na uvuvi usio halali katika maji ya kisiwa cha Madagascar, na wanaelezea Taifa Leo walivyohangaishwa katika jela za nchi hiyo.
“Hatuwezi kuelezea hata mateso tuliyoyapata. Siwezi sema zaidi ila tumeteseka huku tukipata msaada kidogo sana kutoka kwa mamlaka za humu nchini,” akasema Bw Mbarak.
Kwa mujibu wake, kama wageni nchini humo, hawakupata chakula cha kutosha na walikuwa wakiteseka kutokana na kutoelewana lugha katika nchi hiyo.
Wanne hao wameeleza kuwa, waliumilia miezi minne, wakisubiri kuachiliwa huru kwani tofauti na jela za kawaida, walilazimika kujitafutia chakula nje ya jela kwa kuwa hakukuwa na chakula cha kutosha kwa ajili yao.
Waathiriwa hao walisema kuwa , iliwalazimu kuwapigia simu jamaa zao humu nchini ili wawatumie hela ya chakula.
“Kando na chakula, kulala sakafuni kuliniathiri sana na hata sasa mguu wangu hauna hisia. Tangu kukamatwa kwetu, mamlaka ya humu nchini ilitutelekeza, kama siyo shirika la Uchukuzi wa Kimataifa(ITF) tungeozea kwenye jela ya nchi hiyo,” akadokeza Bw Bakari.
Bw Nguma kwa upande wake alieleza kuwa walisalitiwa na mmiliki wa chombo ambaye alitaka kuwatelekeza baada ya Meli yao kukamatwa kwa kuvua papa na samaki wengine ambao ni haramu kuwavua.
“Tumeteseka, kuishi katika hali isiyotamanika katika jela ya wafungwa 503, kama isingekuwa mfungwa mmoja ambaye alikuwa na uwezo wa kuzungumza Kiingereza, tungeteseka hata zaidi kwa kuwa hatukuweza kuzungumza Kifaransa,” akasema Bw Nguma.
Licha ya kuokolewa, familia za wavuvi hao zinalilia fidia na usaidizi wa kisaikolojia kwa mateso waliyopitia nchini Madagascar.
“Tunaomba serikali kuu na taasisi zingine za masuala ya ubaharia iingilie kati na kushinikiza tulipwe hela zetu wajati tulipokuwa gerezani kwa kuwa mwajiri wetu hatumwoni. Anapaswa kulazimishwa kulipa,” akasema Bw Mbarak.
Walieleza kuwa wanaofanya kazi katika sekta hiyo walipaswa kupata vibali vya kuendesha uvuvi, na kuna uwezekano kuwa kwa masaibu waliyoyapitia yangeepukwa.
Meli hiyo ilishikwa na wavuvi wanane Wakenya watatu, na Wasirilanka watano, ikiwa na kilo 5,210 za papa, kilo 135 za papa waliohifadhiwa kwa chumvi, na samaki wengine kinyume na kipengee cha sheria ya uvuvi ya Madagascar, katika maji yake bila kibali.
Waziri wa Uchumi wa majini Bw Hassan Joho, alikuwa ametoa onyo kwa taasisi zilizokuwa zikifeli katika kutekeleza wajibu.
Bw Joho alijihusisha katika juhudi mbalimbali zilizohakikisha wavuvi hao wameachiliwa huru, taasisi mbalimbali zikihusishwa kuhakikisha wameachiliwa upesi.
Afisa wa ITF alieleza taasisi mbalimbali za serikali zilipaswa kuungana kuepuka kama visa kama hivi katika siku za usoni.