Dimba

Man U wanunua mabeki wawili kwa mpigo

August 14th, 2024 2 min read

MANCHESTER, Uingereza

MANCHESTER United imetumia zaidi ya Sh10 bilioni kuwanasa mabeki Matthijs de Ligt na Noussair Mazraoui kutoka Bayern Munich ya Ujerumani, huku kocha Eric ten Hag akitumai watakuwa tayari kucheza kesho nyumbani dhidi ya Fulham katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

De Ligt aliye na umri wa miaka 25 amemwaga wino katika mkataba wa miaka mitano huku Mazraoui akisaini miaka minne, yote ikiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.

Wawili hao wameungana tena na kocha Eric ten Hag aliyekuwa kocha wao katika klabu ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi iliyofika nusu-fainali ya Kombe la Klabu Bingwa barani Ulaya mnamo 2019, mbali na kusaidia Ajax kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredevise).

De Ligt alijiunga na Juventus mnamo 2019 na kuisaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) pamoja na Kombe la Coppa Italia. Hatimaye, alijiunga na Bayern mwaka 2022 na kuichezea mechi 73, mbali na kuisaidia kushinda ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

“Hag alichangia pakubwa kuimarisha kiwango changu cha mchezo na daima siwezi kukawia kuitika wakati wowote kila atakaponihitaji. Niko tayari kusaidia United kushinda mataji,” aliongeza.

Mazraoui kwa upande wake alisema: “Nimejawa na furaha kuungana tena na Hag. Naelewa mfumo wake wa uchezaji tangu nikiwa na umri mdogo.”

Ujio wa Mazraoui umetokana na kuondoka kwa Aaron Wan Bissaka, 26, aliyejiunga na West Ham United kwa dau la Sh2.4 bilioni. Mwingereza huyo alijiunga na Manchester United mnamo 2019 akitokea Crystal Palace.

Wakati huu ambapo shughuli za usajili zinaendelea, vile vile Manchester United imeripotiwa kuendelea kumfuata beki Jarrad Branthwaite, baada ya ofa yao kukataliwa mara mbili.

Palmer

Wakati huo huo, kiungo mshambuliaji Cole Palmer wa Chelsea amerefusha mkataba wake kuendelea kuchezea klabu hiyo ya EPL.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 aliifungia Chelsea mabao 25 na kusuka pasi 15 zilizochangia mabao katika mechi 45 tangu asajiliwe akitokea Manchester City.

Kwa mujibu wa mkataba wa sasa, Mwingereza huyo atakuwa Stamford Bridge kwa miaka tisa, huku marupurupu yake yakiongezeka kutokana na kiwango chake kizuri cha uchazaji.

Palmer ni miongoni mwa wachezaji wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora wa PFA, Mchezaji Bora wa Umri Mdogo ambazo zitatolewa juma lijalo mjini Salford, siku chache tu baada ya awali kuibuka mshindi wa Mchezaji Bora wa EPL msimu wa 2023/2024.

Kiungo huyo ni miongoni mwa watakaotegemewa Jumapili Chelsea chini ya kocha mpya Enzo Maresca itakapokomoana na Manchester City.