Maoni: Wakazi wa Kisumu wahame ODM kwa kuzidi kupuuzwa
KINARA wa Upinzani Raila Odinga na Rais William Ruto wanastahili wahakikishe kuwa Kaunti ya Kisumu inapata uwaziri kutokana na mchango na umuhimu wake kwenye siasa za nchi.
Licha ya kuwa kitovu cha siasa za upinzani na mageuzi nchini, kwa sasa Kisumu haina nafasi yoyote ya hadhi kwenye utawala wa Kenya Kwanza, jambo ambalo huenda halijazoelewa na wakazi wa eneo hilo.
Kwa sasa kiongozi anayeshikilia wadhifa wa hali ya juu kutoka kaunti hii ni Fred Outa ambaye ni balozi wa Kenya kule Misri.
Viongozi wengine ni wabunge, seneta, gavana na mbunge mwakilishi wa kike ambao wote walichaguliwa kupitia ODM kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
Hata hivyo, uwakilishi huu hautoshi kwa sababu eneo kushikilia bendera ya uwaziri, tangu uhuru linahusishwa na hadhi na manufaa tele.
Ni rahisi sana kwa waziri kumfikia Rais moja kwa moja na pia kuwasilisha maslahi ya eneo lake hasa kwenye mikutano ya baraza la mawaziri.
Wakati ambapo mabadiliko yalifanyika ya makatibu majuma mawili yaliyopita, nafasi ya katibu iliyokuwa ikishikiliwa na mtu kutoka Kaunti ya Kisumu ilichukuliwa na kuishia Siaya.
Aliyekuwa Katibu katika wizara ya uchukuzi Alfred KÓmbundo ambaye anatoka Kisumu aliondolewa kwenye wadhifa huo na kuteuliwa naibu balozi huku nafasi yake ikipokezwa Regina Orege kutoka Siaya.
Wakati ambapo mabadiliko madogo yalifanyiwa baraza la mawaziri wiki jana, Kisumu pia ilikosa kupokezwa chochote licha ya kushabikia sana ushirikiano wa Rais Ruto na Bw Odinga.
Mawaziri John Mbadi (Fedha) na Opiyo Wandayi (Kawi) nao wanatoka Homa Bay na Siaya mtawalia huku Kisumu ikiendelea kubakia tu kama watazamaji.
Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor naye ni mzaliwa wa Kisumu lakini ameolewa Siaya wala wadhifa anaoushikilia hauwezi kunasibishwa na Kisumu.
Pili, inashangaza kuwa hata wakati ambapo nyadhifa zilikuwa zikigawanywa kwenye uongozi wa ODM, Kisumu ilisahaulika huku Homa Bay na Migori zikinufaika.
Uenyekiti wa ODM uliendea Homa Bay (Gladys Wanga) na pia Kiranja wa wachache Millie Odhiambo anatoka kaunti hiyohiyo.
Kiongozi wa wachache Bungeni Junet Mohamed naye anatoka Migori.
Isitoshe, wakati ambapo nyadhifa za kamati za bunge zilikuwa zikigawanywa kama ishara ya mlahakama mzuri kati ya ODM na Kenya Kwanza, ni mbunge wa Seme James Nyikal pekee ndiye alinufaika kwa kupokezwa uenyekiti wa kamati ya afya.
Iwapo Kisumu itaendelea kupigwa kumbo wakati ambapo teuzi muhimu zinafanywa serikalini, basi wakazi wake wanastahili kutafakari upya kuhusu uungwaji mkono wao kwa ODM.
Kisumu ndio kitovu cha siasa Nyanza na Kenya na wameshiriki maandamano yote yaliyohusishwa na ukombozi wa nchi.
Kando na kuwa majemedari wa Raila, maamuzi muhimu ya kutoa mwelekeo kuhusu uongozi wa nchi huwa yanafanywa Kisumu.
Isitoshe, Kisumu ndio makao makuu kwa jamii ya Waluo kutoka Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na ukanda wote wa Afrika Mashariki.
Itakumbukwa hata tamasha shirikishi ya jamii hiyo iliandaliwa Siaya mwaka jana, 2024.
Hizi sifa zote na mchango aula wa Kisumu, mbona bado ipigwe kumbo wakati wa uteuzi wa mawaziri?
Mombasa ambao ni sako kwa bako na Kisumu kihadhi wana Salim Mvurya na Hassan Joho kama mawaziri.
Wakati umefika ambapo utawala huu unastahili kuthamini wakazi wa Kaunti ya Kisumu, na eneo hilo lipokezwe uwaziri.