Habari za Kitaifa

Maswali mengi Miano akikosekana orodha, Ruto akibadilisha Duale na Tuya kabla msasa Bungeni

Na SAMWEL OWINO July 24th, 2024 1 min read

KATIKA mabadiliko nadra sana, jana Rais William Ruto alimteua Bi Soipan Tuya kama Waziri wa Ulinzi badala ya Bw Aden Duale ambaye sasa atasimamia wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Uhifadhi wa Misitu.

Mabadiliko hayo yako katika barua ya Rais kwa bunge akiomba mawaziri wateule kuidhinishwa.

Alipotaja nusu ya mawaziri wake Ijumaa, Rais alimteua Bw Duale kama Waziri wa Ulinzi huku akimteua Bi Tuya kuendelea kusimamia wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Misitu.

Katika orodha hiyo, jina la Rebecca Miano, aliyeteuliwa Mwanasheria Mkuu lilikosekana. Mawasiliano hayo ambayo yalishangaza Bunge yaliwafanya wabunge hao kupiga kelele wakimtaka Spika kuripoti.

“Tuna shaka ikiwa hii ndiyo habari ya kweli au la. Ningependa kuwaambia wenzangu kuwa mara hii, msasa wa wateule hawa hautakuwa kama kawaida, safari hii, kama mtu hafai na hana uwezo, tutamtupa nje, Bw Spika,” alisema Kiranja wa Wachache Junet Mohamed.

Mbunge wa Tiaty William Kamket alisema, “Ulichosoma kinakinzana na kile ambacho Rais alitangaza, ningependa uthibitishe kwamba ulichosoma ndicho kilichowasilishwa na Rais. Hata kama kiwango kinafaa kuwa cha juu kwa yeyote anayeteuliwa waziri, huwezi kutarajia Rais kuteua malaika katika Baraza la Mawaziri. Bw Mohamed hafai kutishia kazi za wengine,” Bw Kamket alisema.

Bw Duale alitumia akaunti yake ya X kusema anashukuru kwa kukabidhiwa wizara nyingine.

“Ninatazamia kuhudumu katika wizara mpya na kuhakikisha usimamizi endelevu wa mazingira, kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa na kukuza uhifadhi misitu kwa kupanda miti kwa bidii,” Bw Duale alisema.