Habari Mseto

Mfanyabiashara avua nguo kortini


MFANYABIASHARA alishtua na kushangaza mahakama ya Milimani Jumatano alipovua jaketi kuonyesha jinsi shati yake ilivyoraruliwa na dereva wa Uber alipodai amlipe Sh7,000 badala ya Sh900.

Ajeshi Shireta mwenye umri wa miaka 52 alihoji uadilifu wa polisi walioshuhudia akichapwa na kuraruliwa shati na Eliakim Ombati mnamo Julai 14, 2024 katika eneo la Parklands.

“Mheshimiwa ona shati langu. Limeraruliwa vipande. Nilichapwa huku polisi wakiangalia. Hawakumchukulia hatua yoyote Ombati licha ya kunirarulia shati,” Shireta alifichua kilichojiri katika kituo cha polisi cha Parklands mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Robinson Ondieki.

Mshtakiwa anayefanya kazi katika kiwanda kimoja katika barabara ya Mombasa alimweleza Bw Ondieki, “Ona shati langu Mhehshimiwa nilipigwa na Ombati. Shati langu liliraruliwa. Hakuna hatua iliyochukuliwa na polisi.”

Shireta alieleza mahakama kwamba alichapwa na Ombati akimtaka amlipe Sh7,000 badala ya Sh900.

“Polisi waliangalia tu nikichapwa. Ombati alinichukua kwa gari lake la Uber kutoka Kawangware hadi Parklands kwa bei ya Sh900. Lakini tulipofika Parklands Ombati aligeuka kisha akadai malipo zaidi,” Shireta alimweleza hakimu.

Pia alisema tangu alipokamatwa yapata siku tatu watu wa familia yake hawajui alipo.

Aliomba aachiliwe kwa dhamana ya aidha Sh10,000 ama Sh15,000 akisema “hana simu wala hakumbuki nambari ya simu ya mtu yeyote wa familia yake.”

Kiongozi wa mashtaka Everlyne Mutisya hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Bw Ondieki alimwachilia Shireta kwa dhamana ya Sh40,000.

Hakimu aliamuru kesi hiyo itajwe katika muda wa wiki mbili kuwezesha Bi Mutisya amkabidhi nakala za mashahidi.