AFCON: Mastaa watakaokosekana uwanjani na sababu zao
Na GEOFFREY ANENE
KAMA wewe ni shabiki wa Pierre-Emerick Aubameyang, Joel Matip, Emmanuel Adebayor na Gervinho jua kwamba utahitajika kutafuta mchezaji mwingine wa kushabikia kwenye Kombe la Afrika (AFCON) kwa sababu wako katika orodha ya wachezaji nyota ambao pia watakuwa mashabiki nchini Misri kutoka Juni 21 hadi Julai 19, 2019.
Mshambuliaji wa Arsenal, Aubameyang, ambaye aliibuka mfungaji bora kwenye Ligi Kuu ya Uingereza msimu 2018-2019 kwa mabao 22 kwa pamoja na nyota wa Liverpool Mohamed Salah na Sadio Mane, hakuweza kusaidia Gabon kujikatia tiketi ya kuwa nchini Misri.
Gabon ilikuwa kundi moja na Mali na Burundi zilizonyakua tiketi, na Sudan Kusini.
Matip, ambaye alichezea Indomitable Lions ya Cameroon mara moja pekee tangu mwaka 2014, aliendelea kukataa mwito hata baada ya tetesi kwamba alitumiwa ujumbe kumuomba abadili msimamoa wake wa kutaka kuchezea klabu yake ya Liverpool pekee.
Gervinho aling’ara akiwa Arsenal miaka iliyoenda. Pia, aling’aa akichezea Parma kwenye Ligi Kuu ya Italia msimu 2018-2019 hata kutiwa katika kikosi cha Ivory Coast.
Hata hivyo, alitemwa dakika ya mwisho pale kocha Ibrahim Kamara alipoamua pengine muda wake katika timu ya taifa umeisha kwa kumuacha nje ya kikosi chake cha mwisho cha wachezaji 23.
Hii hapa orodha ya baadhi ya wachezaji nyota ambao watakosekana katika AFCON 2019:
Vincent Aboubakar (Cameroon) – mkekani akiuguza jeraha
Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon) – Gabon haikufuzu
Gervinho (Ivory Coast) – alitemwa
Kelechi Iheanacho (Nigeria) – alitemwa
Juma Balinya (mfungaji bora Ligi Kuu Uganda) – alitemwa
Allan Wanga (Kenya) – alitemwa
Joel Matip (Cameroon) – alikataa mwito
Eric Bailly (Ivory Coast) – jeraha
Emmanuel Adebayor (Togo) – Togo haikufuzu
Aristide Bance (Burkina Faso) – Burkina Faso haikufuzu
Itumeleng Khune (Afrika Kusini) – jeraha
Jeffrey Schlupp (Ghana) – jeraha
Fashion Sakala (Zambia) – Zambia haikufuzu
Jacques Tuyisenge & Meddie Kagere (Rwanda) – Rwanda haikufuzu