Gor, Ulinzi wavuna ushindi mkubwa, Tusker ikijikwaa KPL
GOR MAHIA Jumapili ilinyeshea Mara Sugar 4-0 katika uga wa Dandora jijini Nairobi na kurejelea ushindi huku Tusker ikiponza nafasi ya kupaa kileleni mwa Ligi Kuu (KPL).
Tusker, mabingwa mara 13, walipata pigo baada ya kupoteza uongozi wa 1-0 na kuchapwa 2-1 na Mathare United kwenye mechi ya mapema iliyosakatwa uga huo huo wa Dandora.
Katika mechi nyingine Jumapili, Ulinzi Stars ilipata ushindi mkubwa huku ikiipiga FC Talanta 4-0 kwenye uwanja wa Ulinzi Sports Complex mtaani Lang’ata. Katikati mwa wiki jana, FC Talanta iliwashangaza wengi kwa kupiga Gor Mahia 1-0 uwanjani Dandora.
Aidha Kakamega Homeboyz iliponza nafasi ya kuendelea kupanda nafasi za juu KPL baada ya kuaga sare tasa dhidi ya Sofapaka kwenye uwanja wa Mumias Sports Complex, Kaunti ya Kakamega
Ugani Dandora, Gor ilitawala mchuano huo na kuvuna ushindi mkubwa kupitia mabao ya Shariff Musa, Enock Morisson, Gideon Bendeka na Alpha Onyango.
Kupata huku alama tatu kulikuwa kutamu ikizingatiwa Gor ilikuwa imepata sare ya 1-1 dhidi ya Sofapaka kabla ya kupigwa 1-0 na FC Talanta katikati mwa wiki
Ushindi huo uliongeza alama ambazo Gor imejikusanyia msimu huu hadi alama 50 baada ya mechi 28. Zikiwa zimesalia mechi sita msimu huu utamatike, Kenya Police inaongoza kwa alama 52 kisha Tusker ikiwafuata kwa alama 51.
Kocha wa Gor Mahia Sinisa Mihic alikuwa amerejea kwenye benchi ya kiufundi baada ya kukosa mechi za Sofapaka na FC Talanta kutokana na marufuku aliyopigwa kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya KCB mnamo Aprili 7.
Wikendi inayokuja, Gor itakuwa na kibarua kikali, ikitarajiwa kupambana na nambari nne Shabana (alama 46) uwanjani Gusii, Kaunti ya Kisii.
Ugani Dandora, mvamizi raia wa Uganda Deogratious Ojok aliwapa Tusker uongozi kipindi cha kwanza lakini Musa Masika akafunga mawili kwa Mathare United, moja kupitia mkwaju wa penalti na kupunguza kasi ya vijana wa Kocha Charles Okere ligini.
Winga Boniface Muchiri, Meshack Karani, Amatton Samunya na Joseph Ochieng walifungia Ulinzi Stars mabao yao dhidi ya FC Talanta.
Licha ya kuselelea eneo hatari la kushushwa ngazi kwa kipindi kirefu, Ulinzi sasa wapo nambari 11 kwa alama 35 baada ya mechi 29 huku FC Talanta ikiwa pabaya, nambari 15 kwa alama 29 baada ya mechi 29.