Michezo

Guu niponye kwa Gor, Police, na Tusker KPL ikiyoyoma

Na CECIL ODONGO May 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KASI ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu (KPL) inaingia hatua muhimu Jumatano na Alhamisi katika mkumbo wa 31 huku Kenya Police, Tusker na Gor Mahia wote wakipambana kwa jino na ukucha kusaka ushindi.

Kenya Police wanaoshikilia uongozi kwa mwanya wa alama tatu, zikiwa zimesalia mechi nne msimu uishe, wako pazuri kuwahi ubingwa iwapo watapata ushindi leo katika mechi zao zilizosalia.

Police wana alama 58, tano mbele ya Tusker huku Gor ikiwa na alama 53 lakini ikiwa imesalia na mechi tano.
Tusker na Kenya Police walikuwa na michuano wikendi na wakashinda mechi zao zote.

Hata hivyo, Gor walipumzika vya kutosha baada ya debi ya Mashemeji dhidi ya AFC Leopards kuahirishwa kutokana na ukosefu wa uwanja.
Shabana na Kakamega Homeboyz ambao wamekusanya alama 49 na 48 mtawalia kihisabati bado wako kinyang’anyironi ila wana nafasi finyu ya kutwaa ubingwa huo.

Mechi za katikati ya wiki zitanogesha ubingwa huku Kenya Police ikivaana na KK Homeboyz ugani Mumias Sports Complex nao Tusker wakiitembelea FC Talanta ugani Dandora.

Alhamisi, Gor nao wanatarajiwa kuwa na wakati rahisi kupiga wavuta mkia Nairobi City Stars, wakilenga kupunguza mwanya wa alama kati yao na Tusker na Kenya Police.

Wakilenga ubingwa wao wa kwanza, Kenya Police wamebaki na Homeboyz, FC Talanta, Shabana na Gor Mahia. Msimu uliopita, walimaliza nafasi ya tatu kwa alama 57 nao msimu wa 2022/23 pia walimaliza nambari hiyo hiyo kwa alama 64. Msimu wa 2021-22 walimaliza nambari tisa kwa alama 47, msimu huo huo ambao walipandishwa KPL.

Hii ina maana kwamba wakiwa na alama 58, tayari wamepita idadi ya alama walizopata 2021/22 na msimu ulopita. Iwapo watashinda mechi zote nne, watakuwa na alama 70, alama zaidi ambayo wamejikusanya KPL. Hata hivyo, mechi yao dhidi ya Kakamega Homeboyz haitakuwa rahisi.

Katika mechi saba zilizopita kati ya timu hizo mbili, Homeboyz imeshinda mara mbili, Kenya Police mara tatu kisha mechi mbili zimeishia sare.
Dhidi ya Homeboyz watakuwa wakitegemea Mohamed Bajaber na Clinton Kinanga kuwafungia magoli.

Wikendi iliyopita kiungo Marvin Nabwire alifunga bao la dakika ya 92 dhidi ya Bandari na kuepusha Kenya Police na sare.

RATIBA: Leo: FC Talanta v Tusker (Dandora, Nairobi,1pm), AFC Leopards v Mathare Utd (Dandor,4pm), KK Homeboyz v Kenya Police (Mumias SC, 2pm), Shabana v Bidco United ( Gusii, 2pm), Murang’a Seal v Sofapaka (SportPesa Arena, Murang’a 3pm), Mara Sugar v Bandari (Awendo Green, Migori, 2pm)

Ulinzi Stars v Posta Rangers (Ulinzi Complex, 3pm); Kesho: Gor v Nairobi City Stars ( Dandora, 4pm), Kariobangi Sharks v KCB (Dandora, 2pm).