Ingwe hatimaye yapata ushindi, Police, Shabana zikiwika KPL
AFC LEOPARDS Jumamosi ilisitisha rekodi duni ya kutopata ushindi kwenye mechi sita zilizopita huku Kenya Police ikirejea kileleni mwa Ligi Kuu (KPL) kupitia ushindi wa 2-1 dhidi ya KCB ugani Sportpesa Arena, Kaunti ya Murangá.
Ingwe ilinyorosha Bidco United 3-1 katika uga huo huo wa Dandora mechi ambayo ilianza saa 10 jioni.
Shabana nao waliendelea kukwea jedwali la KPL, wakifunga Nairobi City Stars 2-0 uwanja wa Kenyatta, Kaunti ya Machakos.
Kwenye mechi nyingine Kariobangi Sharks walikemewa na Kocha William Muluya wakipigwa 2-1 na Bandari katika uga wa Dandora.
Murangá Seal ipo pabaya kuondolewa KPL mwishoni mwa msimu iwapo hawatayapata matokeo mazuri. Timu hiyo ilipigwa 3-2 na Posta Rangers kwenye mchuano uliogaragazwa pia katika uga wa Kenyatta.
Ingwe haikuwa imepata ushindi kwa kipindi kirefu lakini mashabiki wao waliojaa ugani Dandora walijawa na tabasamu huku Christopher Koloti akifunga magoli mawili na Kennedy Owino akiongeza jingine. Bao la Bidco la kufutia machozi lilipachikwa wavuni na Simon Abuko.
Ushindi huo uliwapaisha Ingwe, mabingwa mara 12 wa KPL, hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la KPL kwa alama 41 baada ya mechi 28
Kenya Police waliipiku Tusker kileleni, wakiwa na alama 52 kutokana na mechi 28. Tusker wanacheza Jumapili dhidi ya Mathare United ugani Dandora na watarejea juu wakishinda.
Mabao mawili ya Kenya Police dhidi ya KCB yalititigwa nyavuni na David Owino huku Patrick Otieno akifungia wanabenki hao. Zikiwa zimesalia mechi sita msimu ukamilike, KCB wapo nambari sita kwa alama 41.
Tore Bobe iliendelea kujiandalia Gor Mahia wikendi ijayo, Keith Imbali na Darius Msagha wakihakikisha wananyanyasa City Stars ambao wanakumbwa na uchechefu wa kifedha na wapo mkia wa KPL.
Shabana pia wanalisaka taji wakiwa nambari nne kwa alama 46, moja nyuma ya mabingwa watetezi Gor ambao wanavaana leo dhidi ya Mara Sugar ugani Dandora.
“Waliingia kwa mtego wetu, tukajidhari wasitufunge na sisi tunalenga kufunga na kushinda mechi zetu. Hatujakutana na Gor na Tusker ambao wapo juu na lazima tuwashinde kwa hivyo, hata nasi tunawania ubingwa wa KPL,” akasema Kocha wa Shabana Peter Okidi.