Itakugharimu Sh33,000 kuvaa kiatu spesheli cha hotshot Yamal wa Barcelona
ITAKUGHARIMU Sh33,603 (Dola za Amerika 260) kupata daluga za Adidas zilizo na nembo ya chipukizi matata wa Barcelona, Lamine Yamal.
Viatu hivyo viko katika rangi za pinki na zambarau ambazo winga huyo raia wa Uhispania alizichagua kwa sababu anazipenda.
Kuna jozi 304 pekee kote duniani za viatu hivyo spesheli kwa jina F50 LY304, ambavyo inatarajiwa tayari vimetua sokoni tarehe hii ya leo Jumatano, Desemba 18 kisha vitafurika soko kwa wingi Januari 2025.
Viatu hivyo vitapatikana katika maduka yanayouza bidhaa za Adidas na pia kwenye tovuti ya Adidas. Viatu hivyo havina kamba. Vilizinduliwa rasmi Jumatatu usiku. Nambari ‘304’ ni nambari tatu za mwisho za anwani ya mji anakotoka Yamal nchini Uhispania.
Mwezi Februari 2024, kampuni ya Adidas kutoka Ujerumani iliipiku kampuni ya Nike ya Amerika na kusaini kandarasi ya muda mrefu na Yamal ambaye anafanya makubwa katika soka.
Manufaa ya kuwa mchezaji aliyesainiwa na Adidas ni pamoja na kujengwa brandi yake kibinafsi. Yamal sasa ana nembo yake, daluga zilizo na akronimi yake pamoja na mkwanja mzito utakaoandamana na kusainiwa kwake.
Wanasoka wengine waliosaini kandarasi na Adidas ni pamoja na supastaa Lionel Messi (Inter Miami & Argentina), mshambulizi matata Mohamed Salah (Liverpool & Misri), na viungo Jude Bellingham (Real Madrid & Uingereza) na Mfaransa Paul Pogba.
Yamal yuko pazuri kuwa balozi mkuu wa daluga za F50 mara tu Messi atakapostaafu.
Yamal, 17, kwa sasa yuko mkekani kwa angaa wiki tatu ama nne akiuguza jeraha la kifundo ambalo alipata wakati Barca waliduwazwa 1-0 na Leganes kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) hapo Desemba 15.
“Mwaka huu umekuwa kama ndoto kwangu na kushirikiana na Adidas kuwa na daluga kwa nembo yangu inafurahisha zaidi. Waliponialika nifanye kazi na madizaina kuwa sehemu ya kukiunda, nilifurahi sana jinsi ilivyokuwa ikiendelea na kuongeza mchango wangu,” akasema Yamal na kuongeza kuwa anasubiri sana kuvaa daluga hizo uwanjani.
Yamal ana mabao matano na asisti 10 kufikia sasa La Liga msimu huu.
Imeandaliwa na GEOFFREY ANENE