Kocha wa Gor awakia ubovu wa uwanja wakiipiga KCB KPL
KOCHA wa Gor Mahia Sinisa Mihic Jumatatu alisema kuwa timu hiyo ipo pazuri kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu (KPL) baada ya kuichapa KCB 1-0 katika uga wa Kenyatta Kaunti ya Machokos Jumatatu asubuhi.
Mchuano huo ambao ulistahili kusakatwa mnamo Jumapili, ulikuwa umeahirishwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha Machakos na kufanya uwanja huo kufurika maji.
Kiungo Austin Odhiambo alifungia K’Ogalo goli la pekee dhidi ya KCB katika mechi hiyo, akifika mabao yake msimu huu hadi manane. Hata hivyo, Mihic amelalamikia ubovu wa uwanja wa Kenyatta akisema Shirikisho la Soka Nchini (FKF) linastahili kupiga marufuku michuano ya ligi kusakatwa ugani humo.
“Huu si uwanja wa kuandaa mechi za KPL kwa sababu upo kwenye hali duni sana. Hata kama tumeshinda, siwezi kufurahi kuwa kikosi changu kimecheza katika uwanja kama huu,” akasema Mihic kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Ushindi huo ulihakikisha kuwa Gor inafikisha alama 46 na imekaribia Kenya Police (49) na Tusker (48) ambazo zimesakata mechi 26 huku Gor ikiwa bado na mechi moja kiporo.
KCB nao bado wapo nafasi ya tano kwa alama 40 sawa na nambari nne Shabana ila wanadunishwa na mabao timu hizo mbili zikiwa zimesalia na mechi nane msimu utamatike.
Ushindani huo unakifanya kinyángányiro cha kutwaa ubingwa wa KPL uwe ngumu ikizingatiwa zimesalia mechi nane kabla ya msimu huu kutamatika.
“Nimekuwa nikisisitiza kuwa tupo kwenye mbio za kutetea ubingwa wetu. Tutaendelea kujituma kwa sababu sasa hivi mechi tisa ambazo tumesalia nazo ni kama fainali kwetu, tutaendelea kupigania taji,” akaongeza Mihic.
Mechi ya Jumamosi ilikuwa ya kwanza baada ya mafarakano kushuhudiwa kwenye kambi ya Gor ambapo Mihic aliwafukuza makocha wasaidizi akidai walikuwa wakimpiga vita vya ndani kwa ndani. Hata hivyo, alibadilisha uamuzi huo, akawasamehe ila akataka kila mmoja wao amakinikie jukumu lake.