Mashabiki wa AFC Leopards kwenye barabara ya Moi Avenue, Nairobi, wakielekea Mashemeji Dabi dhidi ya Gor Mahia awali Januari 2023. PICHA | DENNIS ONSONGO
KOCHA Fred Ambani wa AFC Leopards atalenga kutimiza mambo mawili atakapoongoza kikosi chake dhidi ya mahasimu wakuu Gor Mahia kwenye mechi ya Ligi Kuu (KPL), Jumapili.
Mechi hiyo maarufu kama Mashemeji Dabi itachezewa uwanja wa kitaifa wa Nyayo jijini Nairobi kuanzia saa kumi jioni (4.00pm).
Itakuwa mara ya kwanza Ambani kuongoza Leopards kama kocha kwenye dabi tangu achukue usukani kutoka kwa Tomas Trucha aliyeondoka Novemba iliyopita kufuatia matokeo duni.
Timu hizo zitarudiana April 6, Gor wakiwa wenyeji.
Kocha Fred Ambani wa AFC Leopards katika kikao na wanahabari Ijumaa kuelekea mechi yao ya KPL dhidi ya Gor Mahia – almaarufu Mashemeji Dabi – hapo Jumapili. PICHA | HISANI
Ambani alichezea Leopards kati ya 1997 hadi 2002 kama mshambulizi, muda ambao Ingwe haikuwahi kushindwa na K’Ogalo.
Sasa kama kocha wa Ingwe amesema tayari amejulisha kikosi chake kwamba angependa kuendeleza rekodi hiyo.
“Nimewaambia sikuwahi kupoteza dabi kama mchezaji na siwezi kupoteza kama kocha,” alisema Ambani kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyiika katika uwanja huo wa kitaifa, Ijumaa.
Kulingana na rekodi za KPL, dabi ya kesho ni ya 96 baina timu hizo tangu 1968. Gor Mahia wanajivunia ushindi mara 33 dhidi ya 28 za Leopards, mechi 34 zikimalizika katika sare.
Mechi hii imekubaliwa kuchezewa Nyayo lakini kwa masharti magumu ya kiusalama kutoka kwa mwenyekiti wa Kamati Andalizi ya Kitaifa ya Fainali za Kombe la CHAN.
Akitoa onyo kali mapema wiki hii mwenyekiti wa kamati hiyo, Nicholas Musonye alisisitiza kwamba timu hizo zitapigwa marufuku kuchezea uwanjani humo hadi baada ya Afcon 2027 iwapo kutatokea fuzo zozote.
Mashabiki wa Gor Mahia kwenye barabara ya Moi Avenue, Nairobi, wakielekea Mashemeji Dabi dhidi ya AFC Leopards awali Oktoba 2023. PICHA | SILA KIPLAGAT
Mechi hii imeahirishwa mara mbili tangu mwaka jana kutokana na ukosefu wa uwanja kwani Nyayo na Kasarani zimekuwa zikiboreshwa kwa ajili ya Dimbla la Afrika kwa Wanasoka wa Ligi za Nyumbani (CHAN) na Kombe la Afrika (AFCON) 2027.
Lakini uga wa Nyayo ulifunguliwa wiki chache zilizopita baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuridhishwa na ukarabati wake.
Tangu ufunguliwe uwanja huo umeandaa mechi mbili za kimataifa za timu za taifa – Junior Starlets vs Tunisia na Harambee Stars vs Gabon.
CHAN ilikuwa imeratibiwa kuanza Februari Mosi mwaka huu ambapo nchi za Kenya, Uganda na Tanzania zitaandaa kwa pamoja. Lakini ikaahirishwa hadi Agosti ili kutoa fursa kwa maandalizi yote kumalizwa kikamilifu.
Katika mechi kadha za Dabi ya Mashemeji zilizopita, Leopards na Gor zimepigwa marufuku kuchezea viwanja fulani kwa sababu ya fuzo za mashabiki wao.
Mnamo Aprili 2024, mashabiki wa timu hizo walisabaisha uharibifu wa mali nyingi katika uwanja wa Nyayo. Leopards ilipigwa faini ya Sh505,450 na kuzimwa kuchezea uwanja huo hadi faini hiyo ilipwe.
Mara ya mwisho Leopards kushinda Gor ilikuwa Mei 2023 huku K’Ogalo ikiibuka kidedea 2-1 na 1-0 katika mechi zilizofuata.