Michezo

Ni wakati wa mastaa wa Harambee Stars kujinadi Kenya ikitoana kamasi na Cameroon

Na GEOFFREY ANENE October 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KIUNGO Timothy Ouma atapata fursa nzuri ya kujinadi kwa maskauti wa Manchester United wakati Harambee Stars watavaana na Indomitable Lions ya Cameroon anayechezea kipa Andre Onana kwenye mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2025 ugani Omnisports Ahmadou Ahidjo mjini Yaounde.

Ouma kutoka klabu ya IF Elfsborg iliyowahi kuajiri beki wa kupanda na kushuka Eric “Marcelo” Ouma, anamezewa mate na klabu kadhaa za Ligi Kuu ya Uingereza zikiwemo Brentford na mashetani wekundu wa United.

Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 20 aliyejiunga na Elfsborg nchini Uswidi mwezi Julai mwaka 2022 akitokea Nairobi City Stars, ametajwa katika kikosi cha wachezaji 24 kwa michuano dhidi ya Cameroon mjini Yaounde hapo Oktoba 11 (Ijumaa) na mjini Kampala, Uganda mnamo Oktoba 14.

Mataifa haya yalikutana katika mechi za kufuzu kushiriki AFCON1998 ambapo walitoka 0-0 mjini Nairobi (Februari 23, 1997) na 1-1 mjini Yaounde (Julai 27, 1997).

Tiketi zinauzwa kwa kati ya Sh430 (Franc 2,000) na Sh10,756 (Franc 50,000). Raia wa Senegal, Issa Sy atakuwa mpuliza kipenga katika mechi kati ya Cameroon na Kenya mjini Yaounde. Kenya haikufuzu baada ya kumaliza ya mwisho katika kundi lake.

Katika mchuano mwingine wa Kundi J, Khama Biliat alifungia Zimbabwe bao la pekee kupitia penalti dakika ya 34 katika ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji Namibia nchini Afrika Kusini, Alhamisi. Zimbabwe wanaongoza kwa alama tano kutokana na ushindi mmoja na sare moja wakifuatiwa na Kenya na Cameroon (ushindi mara moja na sarea moja) nao Namibia hawajapata alama.

Vikosi:

Cameroon

Makipa – Simon Ngapandouetnbu, Simon Omossola, Andre Onana; Mabeki – Christopher Wooh, Jackson Tchatchoua, Enzo Flavien Boyomo, Nouhou Tolo, Michael Ngadeu-Ngadjui, James Ndjeungoue, Guy-Marcelin Kilama, Fai Collins; Viungo – Andre-Frank Zambo Anguissa, Carlos Baleba, Olivier Ntcham, Martin Hongla, Pierre Kunde Malong, Martin Atemengue; Washambulizi – Christian Bassogog, Bryam Mbeumo, Boris Enow, Frank Magri, Vincent Aboubakar, Partick Soko, Nicolas Ngamaleu; Kocha – Marc Brys (Ubelgiji)

Kenya

Makipa – Ian Otieno, Patrick Matasi, Byrne Omondi; Mabeki – Alphonce Omija, Daniel Anyembe, Amos Nondi, Sylvester Owino, Johnstone Omurwa, Collins Sichenje, Joseph Okumu, Geoffrey Ochieng, Eric Ouma; Viungo – Chrispine Erambo, Richard Odada, John Ochieng, Timothy Ouma, Anthony Okumu, Duke Abuya, Ronney Onyango; Washambulizi – John Avire, Michael Olunga, Jonah Ayunga, Adam Wilson, Alfred Scriven; Kocha – Engin Firat (Uturuki)