Michezo

Ronaldo acheka na nyavu na kusaidia Juventus kurejelea Serie A kwa kishindo

June 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

CRISTIANO Ronaldo alifunga bao na kusaidia Juventus kurejelea kampeni za Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Bologna mnamo Juni 22, 2020.

Juventus ambao wanafukuzia ubingwa wa Serie A kwa msimu wa tisa mfululizo, sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 66, nne zaidi kuliko nambari Lazio ambao watakuwa wageni wa Atalanta mnamo Juni 24.

Ronaldo aliwaweka Juventus kifua mbele kupitia penalti iliyotokana na tukio la beki Matthijs de Ligt kukabiliwa vibaya na Stefano Denswil.

Paulo Dybala alipachika wavuni goli la pili la kikosi hicho cha mkufunzi Maurizio Sarri baada ya kushirikiana vilivyo na Federico Bernardeschi kunako dakika ya 36.

Pigo zaidi kwa Juventus hata hivyo ni ulazima wa kukosa huduma za Danilo katika jumla ya mechi mbili zijazo baada ya beki huyo kuonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha pili. Alex Sandro na Mattia de Sciglio ambao ni mabeki wengine tegemeo kambini mwa Juventus tayari wanauguza majeraha.

Hadi waliposhuka dimbani kubaana na Bologna, Juventus walikuwa wamesajili sare tasa katika mechi mbili zilizopita. Walikabwa koo na AC Milan kwenye nusu-fainali ya Coppa Italia kabla ya kubanduliwa kusonga mbele kupitia mikwaju ya penalti. Hata hivyo, walizidiwa maarifa kwa penalti katika fainali iliyowashuhudia wakitoshana nguvu na Napoli mwishoni mwa kipindi cha kawaida cha dakika 90.