Makala

Mtindo wa Raila kusaliti washirika wake waibuka tena akionekana kuvuna asikopanda

Na BENSON MATHEKA July 27th, 2024 3 min read

JUHUDI za kiongozi wa ODM Raila Odinga za kuokoa serikali ya Rais William Ruto aliye katika shinikizo lililosababishwa na maandamano ya vijana, zimefufua mjadala kuhusu mtindo wake wa kusaliti washirika wake wa kisiasa.

Japo si mara yake ya kwanza kuingia katika ukuruba wa kisiasa na serikali baada ya kushindwa katika uchaguzi, ni mbinu yake ya kufanya hivyo inayozua mdahalo hasa wakati huu ambao vijana wanashinikiza utawala bora.

Huku wanaounga serikali wakimtaja kama mzalendo kwa kuokoa nchi wakati wa mizozo mikubwa ya kisiasa, washirika wake wanamuona kama msaliti.

Baada ya wandani wake kuteuliwa mawaziri katika serikali ya Kenya Kwanza ambayo awali alikuwa akiikosoa vikali kwa kubebesha raia zigo la gharama ya maisha, vinara wenza katika muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja One Kenya wamemtaja kama msaliti kwa kuwa walikuwa wameapa kutojiunga na serikali.

Tukio la Jumatano, Rais William Ruto alipowateua washirika wanne wa karibu wa Raila kwenye baraza jipya la mawaziri, lilizidisha mvutano hata ndani ya ODM na Azimio, huku kiongozi wa chama cha Narc Kenya, Martha Karua akiwasilisha notisi ya kujiondoa katika muungano huo.

Kuna ripoti kwamba hatua ya Raila ilinuia kuvunja muungano huo japo anasisitiza wandani wake John Mbadi, Wycliffe Oparanya, Hassan Joho na Opiyo Wandayi waliteuliwa kama watu binafsi na sio kwa uamuzi wa chama.

Kauli za wabunge wa ODM zinaonyesha kuwa ulikuwa uamuzi wa chama hicho cha Chungwa.

“Ninataka nimpongeze Rais kwa uteuzi huo lakini pia ninaomba ndani ya wiki moja, mara tu kesho, tuone majina ya wateule ambao Baba alipeleka leo na tunataka wote wapitishwe, na ikiwezekana basi, hii ifanyike haraka sana. Kama chama cha ODM, tulikaa na kusema serikali ya Kenya ni yetu sote. Tulikutana na kuamua,” mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma alisema Jumanne kabla ya Rais kutangaza majina ya wanachama wa ODM kuwa mawaziri Jumatano.

Karua aliyekuwa mgombea-mwenza wa Raila katika uchaguzi mkuu wa 2022 ambao Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua waliibuka washindi, alisema matukio ya kisiasa nchini yanafanya Narc Kenya kutoendelea kuwa katika Azimio la Umoja.

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2018, Bw Odinga aliwaacha washirika wake katika uliokuwa muungano wa Nasa na kuanza ukuruba wa kisiasa na Rais Uhuru Kenyatta ambaye wadadisi wa siasa wanasema alikuwa mateka wa naibu wake Dkt Ruto.

Hatua yake iliyozaa uhusiano wa kisiasa uliofahamika kama handisheki ilifanya Nasa kusambaratika na kumrahisishia Uhuru muhula wake wa pili, Dkt Ruto akitengwa katika serikali ya Jubilee.

Inasemekana kuwa chini ya ukuruba wake wa kisiasa na Bw Uhuru, alikataa washirika wake kuteuliwa serikalini, jambo ambalo amekubali chini ya usuhuba wake na Rais Ruto.

Akizungumza katika mkutano wa Baraza Kuu la kitaifa la ODM na kundi la wabunge kabla ya wandani wake kuteuliwa mawaziri, Raila alionekana kuunga mkono utawala wa Dkt Ruto akikosoa presha za vijana kutaka Rais ajiuzulu, akisema shinikizo hizo zina athari hasi.

“Ruto aende, basi nini? Ruto huenda akaondoka, kisha Rigathi Gachagua achukue hatamu, bado atatekeleza sera mbovu. Ruto pia anaweza kusema nimechoka, acha majenerali (wanajeshi) wachukue madaraka. Ruto lazima aende, haiwezi kuwa suluhu,” Bw Odinga alinukuliwa akisema siku chache kabla ya Rais kuwateua wandani wake.

“Ni wakati wa shida kama huu ambapo nchi inahitaji kuzungumza. Hatufanyi hivyo ili kumwokoa Ruto. Tunafanya hivyo kuokoa Kenya,” aliongeza.

Kulingana na wadadisi wa siasa, Raila amemuokoa Ruto aliyeonekana kuwa mateka wa naibu wake Bw Gachagua ambaye alikuwa ametangaza serikali ya Kenya Kwanza kuwa ya hisa za jamii na maeneo yaliyoipigia kura kwa wingi.

“Raila Odinga hatabiriki sana kwa sababu unapofikiri kwamba yuko nje, anaibuka tena na mara nyingi, huwapata marafiki zake wa karibu kwa mshangao,” alisema Prof Masibo Lumala wa Chuo Kikuu cha Moi katika mahojiano ya awali.

Kinyume na ilivyokuwa alipomuokoa Bw Uhuru 2018, ukuruba wake na serikali ya Rais Ruto umezua minong’ono katika chama chake, baadhi ya wabunge wake wakieleza kukerwa na uamuzi wa viongozi wao wanne kujiunga na serikali na kupuuza matakwa ya vijana.

“Kwa kuokoa Ruto, sawa na alivyofanya alipomuokoa Uhuru, Raila amesaliti tena washirika wake wa kisiasa na kwa kiwango kikubwa vijana ambao malalamishi yao kwa serikali ni ya kweli. Wanasiasa wenzake wanaweza kumsamehe kwa kuwa hakuna uhasama wa kudumu katika siasa, lakini vijana hawataweza ikizingatiwa ametumia shinikizo zao kwa manufaa ya kibinafsi kujiunga na serikali kupitia washirika wake,” asema Prof Isaac Gichuki.

Wadadisi wanasema Bw Raila pia amemsaliti Uhuru aliyeokoa jahazi lake la kisiasa kabla ya uchaguzi wa 2022 kwa kuunda Azimio, muungano wa Nasa ulipovunjika kufuatia madai Bw Raila aliwasaliti waliokuwa washirika wake wakiwemo Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka na Moses Wetang’ula.