HabariHabari za KitaifaSiasa

Opiyo Wandayi: Sikuomba kazi ya uwaziri, lakini ninafurahi kuteuliwa

Na BENSON MATHEKA August 3rd, 2024 1 min read

WAZIRI mteule wa Kawi na Mafuta James Wandayi amepuuzilia mbali madai kwamba alitumia maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen Z kuomba kazi ya uwaziri.

Akihojiwa na  Kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi hapo Jumamosi, Agosti 3, 2024 Wandayi alifafanua kuwa jina lake liliwasilishwa na mtu mwingine wala si yeye alituma maombi ateuliwe.

Aidha, Wandayi, ambaye alikuwa Kingozi wa Wachache, alisisitiza kwamba licha ya kuteuliwa kuwa waziri bado anaunga mkono masuala yaliyoibuliwa na waandamanaji wanaoipinga serikali.

Wandayi alisema masuala yaliyoibuliwa na vijana hao yalikuwa na umuhimu mkubwa na yanahitaji jibu la haraka kutoka kwa serikali.

Wandayi alisema kuwa baadhi ya malalamishi ya waandamanaji yanawiana na yale wamekuwa wakiibua katika Bunge la Kitaifa.

“Vijana hawakuibua masuala tofauti na yale ambayo tulikuwa tukiibua bungeni. Ni masuala muhimu ambayo lazima yashughulikiwe,” Wandayi alifafanua.

“Hivyo, si sahihi kusema kwamba tulitumia maandamano ya Gen Z ili kupata kazi. Sikuwahi kuomba kujiunga na serikali, lakini nilifurahi jina langu lilipendekezwa,” aliongeza.

Mbunge huyo alimpongeza Rais William Ruto kwa kumteua waziri.

“Bado ninashikilia kwamba hatukusaliti vijana kwa vyovyote vile,” alisisitizia wanakamati.

Wandayi ni miongoni mwa viongozi wanne wa chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement (ODM) walioteuliwa katika nyadhifa za uwaziri na Rais Ruto.