Habari Mseto

Raia wawili wa Nigeria wazuiliwa kwa kuilaghai Text Book Centre

January 24th, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

RAIA wawili wa Nigeria walioshtakiwa kuchukua kwa ulaghai tarakilishi 12 za thamani ya Sh900 milioni kutoka kwa duka la kuuza vitabu la Text Book Centre (TBC), wamezuiliwa gerezani hadi Januari 31, 2024.

Ike Onyekachi na Igwe John Paul walikana mashtaka mawili ya kupokea bidhaa kwa njia ya udanganyifu na kupatikana wakiwa nchini Kenya kinyume cha sheria.

Onyekachi na Igwe walishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Bernard Ochoi na kukana mashataka yaliyowakabili.

Upande wa mashtaka unaoongozwa na Bw James Gachoka ulieleza hakimu mnamo Januari 16 2024 katika TBC walijipatia laputop 12 miundo mbali mbali wakidai walikuwa na uwezo wa kuzilipia.

Thamani ya laputop (tarakilishi) hizo ni Sh942,999.

“Mlieleza wasimamizi wa TBC kwamba mmeweka pesa katika akaunti yake katika benki ya Stanbic Bank of Kenya Limited, mkijua mnadanganya. Ni kweli au sio ukweli,” hakimu aliyewasomea mashtaka aliwauliza wageni hao.

“Sio ukweli,” wawili hao walijibu kwa lugha ya ung’eng’e.

Shtaka la pili dhidi yao lilisema walipatikana madukani ya Hurlingham bila vibali halisi kinyume cha sheria ilhali wao ni raia wa Nigeria.

Wakili anayewatetea washtakiwa hao aliomba wazuiliwe hadi Januari 31, 2024, kumwezesha kupata stakabadhi halisi kutoka ubalozi wa Nigeria nchini.

Bw Gachoka hakupinga ombi washtakiwa wazuiliwe hadi Januari 31, 2024.

“Sipingi ombi kwamba washtakiwa wazuiliwe hadi Januari 31, 2024. Upande wa mashtaka utakuwa unapinga vikali washtakiwa hawa wakiachiliwa kwa dhamana. Afidaviti inayosimulia sababu za kupinga dhamana ya Igwe na Onyekachi imewasilishwa kortini,” alisema Bw Gachoka.

Hakimu aliamuru washtakiwa wazuiliwe hadi mwisho wa mwezi.

“Mtazuiliwa hadi Januari 31, 2024, ripoti kuhusu pasipoti zenu iwasilishwe kortini,” Bw Ochoi aliwaeleza washtakiwa.

Onyekachi na Igwe waliondolewa kizimbani kisha wakaabiri basi la idara ya magereza kupelekwa gereza la Industrial Area kuzuiliwa kule hadi watakaporudishwa tena mahakamani.

Washtakiwa walikana kutekeleza uhalifu huo Januari 16 na Januari 18, 2024, mtawalia.