Habari za Kitaifa

Raila njiapanda kisiasa kuhusu ushirikiano wake na Rais Ruto


KIONGOZI wa Azimio Raila Odinga amejipata katika njia panda kisiasa kutokana na ushirikiano wake na utawala wa Rais William Ruto.

Jumanne, Julai 16, 2024 Bw Odinga ambaye pia ni kiongozi wa ODM alishambuliwa kwenye mitandao ya kijamii kutokana na hatua yake ya kuunga mkono mdahalo ulioitishwa na Rais Ruto kushughulikia malalamishi yaliyoibuliwa na vijana wa Gen-Z.

Dkt Ruto na Bw Odinga wanaunga mkono mdahalo huo wa siku sita uliotarajiwa kuanza mnamo Jumatatu, Julai 15.

Jumla ya washiriki 150 wameratibiwa kushiriki mdahalo huo, 50 miongoni mwao wakiwa vijana na wengine 100 wakiwakilisha wadau mbalimbali.

Bw Odinga anajipata katika hali ambayo sharti aunge mkono matakwa ya serikali kwa sababu anahitaji uungwaji mkono kutoka kwa Rais Ruto katika azma yake ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Anahisi kuwa akifuata mkondo tofauti na Rais Ruto, hatua hiyo itafifisha nafasi yake kushinda wadhifa huo wenye ushawishi mkubwa.

Isitoshe, Bw Odinga pia hajashughulikia changamoto ya urithi katika chama chake ambapo manaibu wake Hassan Joho na Wycliffe Oparanya wanawania kumrithi endapo atashinda kiti AUC.

Waziri huyo mkuu wa zamani pia amejipata njia panda kuhusu suala la chama chake kushirikishwa katika Serikali mpya ya Muungano wa Kitaifa (GNU), wazo linaloungwa mkono na baadhi ya wandani wake na maafisa wa serikali.

Fununu za kuundwa kwa serikali hiyo ya muungano zilijiri baada ya Rais Ruto kudokeza kuhusu nia ya kuundwa kwa “serikali itakayoakisi uwakilishi mpana wa kutoka mirengo mingine ya kisiasa”.

Rais alisema hayo Jumanne baada ya kutia saini Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itakayotoa nafasi ya kuteuliwa kwa makamishna wapya wa tume hiyo.

Duru katika kambi ya Bw Odinga zinasema kuwa ushirikiano kati ya mwanasiasa huyo na Rais Ruto utakuwa tofauti kabisa na uhusiano wake na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kupitia mwafaka uliojulikana kama “Handisheki”.

Hii ni kwa sababu uhusiano wa sasa unahusisha kushirikishwa, moja kwa moja, kwa viongozi wa upinzani serikalini.

Wakati wa serikali iliyopita, Bw Odinga aliunga mkono serikali ya Bw Kenyatta “kutoka nje”.

Mara si moja, Bw Kenyatta alimtaja kiongozi huyo wa ODM kama “mshauri kuhusu namna ya kuendesha serikali”.

Hii ni baada ya Dkt Ruto (ambaye wakati huo alikuwa Naibu Rais) kudaiwa kutelekeza majukumu yake.

Lakini Jumatano, Bw Odinga alisema amepokea jumbe kutoka kwa baadhi ya wanachama wa ODM na idadi kubwa ya Wakenya wanaopinga “handisheki” yake na Rais Ruto.

“Nimeambiwa na hawa viongozi kwamba mmesema hamtaki handisheki. Ujumbe umefika,” akasema kupitia akaunti yake ya X (awali Twitter).

Bw Odinga alisema hayo baada ya kukutana na baadhi ya viongozi wa ODM wenye umri mdogo kama vile, Maseneta Edwin Sifuna (Nairobi), Eddy Oketch (Migori) na Seneta Maalum Crystal Asige.