Habari za Kitaifa

Seneta maalum aomba ada za biashara kupunguzwa  

Na WINNIE ATIENO August 16th, 2024 1 min read

SENETA mmaalum Bi Miraj Abdhalla amelisihi Baraza la Magavana (CoG) kupunguza ada za kufanya biashara katika serikali za kaunti ili kupiga jeki biashara zao.

Bi Abdhalla alisema juhudi hizo zitasaidia vijana kujikimu katika sekta ya biashara na kupata ajira.

Mwanasiasa huyo aliahidi kufanya kikao na Baraza la Magavana linaloongozwa na Anne Waiguru, kama mwenyekiti, alisema vijana wengi ambao hawana ajira wanafaa kutumia biashara kama kitega uchumi.

Bi Waiguru pia ni Gavana wa Kaunti ya Kirinyga.

“Vijana wajasiriamali wameomba magavana kuwaondolea kodi za biashara ili waweze kutega uchumi. Ninawaomba magavana wote nchini kupitia baraza lao kuwapatia vijana muda wa miezi mitatu wasilipe ushuru hadi biashara zao ziimarike,” alisema Bi Abdhalla.

Alisihi vijana kuchukua mikopo kama mitaji ya biashara katika taasisi mbalimbali za kiserikali, ikiwemo, kutoka kwa Hazina Hustler Fund badala ya kulalamika ukosefu wa fedha.

Bi Abdhalla vilevile alihimiza vijana kutumia mitandao ya kijamii kusaka ajira na kujikimu kimaisha.