Habari za Kitaifa

Serikali haina nia ya kukodisha uwanja wa JKIA, Mudavadi asema


MKUU wa Mawaziri Musalia amepuuzilia mbali madai kuwa serikali inapanga kukodisha Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kampuni moja ya India.

Bw Mudavadi Julai 23, 2024 aliwaambia wabunge wanachama wa Kamati ya Fedha katika majengo ya bunge kwamba uamuzi kama huo sharti uidhinishwe kwenye kikao cha bunge lote.

“Ningependa kuweka wazi kwamba hakuna mpango wa kuuza au kukodi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta. Ni mali muhimu zaidi ya umma. Haiwezi kukodishwa bila utaratibu wa sheria kufuatwa na bunge hili kutoa idhini,” akawaambia wanachama wa Kamati wakiongozwa na mwenyekiti wao, Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

Bw Mudavadi alisema hayo siku chache baada ya Seneta wa Kisii Richard Onyanka kudai kuwa Mamlaka ya Kusimamia Viwanja vya Ndege Nchini (KAA) imetia saini mkataba na kampuni ya Adani Airport Holding Ltd kukodi uwanja wa JKIA kwa kipindi cha miaka 30.

Chini ya mkataba huo, Bw Onyonka alidai, kampuni hiyo itaiboresha miundo msingi katika uwanja huo na kuendesha shughuli zake zote.

“Chini na mkataba huo kampuni ya Adani itapata haki ya kuweka ada zitakazolipwa na mashirika mengine ya ndege na watumiaji wengine wa huduma zake katika JKIA,” akaongeza.

Bw Onyonka aliitaka Kamati ya Seneti kuhusu Uchukuzi kutoa taarifa kuhusu yaliyomo kwenye mkataba huo kati ya Adani na JKIA.

Aidha, seneta huyo aliitaka Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Kiambu Karungo Wa Thang’wa kubaini sababu iliyopelekea mkataba huo “kutiwa saini kisiri ilhali JKIA ni mali ya Wakenya.”

Lakini Jumanne Bw Mudavadi akasema hivi: “Mtu yeyote anayeeneza madai kuwa mipango ya kukodisha uwanja huo wa ndege hasemi ukweli. Kile ambacho serikali inafanya sasa ni kutafuta fedha za kuboresha uwanja wetu wa JKIA kwa kujenga vitengo vingine vya abiria kutumia wanapopanga kuabiri ndege,” Bw Mudavadi akasema.