Habari

Shilingi yadumisha uthabiti dhidi ya dola licha ya hadhi ya Kenya kiuchumi kushuka

Na BENSON MATHEKA July 17th, 2024 2 min read

SHILINGI ya Kenya ilisalia thabiti wiki jana dhidi ya dola, ikichochewa na mapato kutoka kwa sekta ya utalii na kilimo licha ya Kenya kushushwa hadhi na Shirika la Kimataifa la Kukadiria Uchumi wa Nchi la Moody na kutimuliwa kwa Baraza la Mawaziri huku maandamano dhidi ya Serikali yakiendelea.

Benki za biashara zilibadilisha Dola ya Amerika kwa Shilingi 128.00/129.00, ikiimarika kutoka 129.50/130.50.

Kulingana na wachanganuzi, kulikuwa na mahitaji makubwa ya fedha za ndani huku watalii wanaozuru Kenya wakitaka kubadilisha dola zao kwa shilingi za Kenya.

Ongezeko hili la mahitaji lilichangia uhaba wa shilingi, ambao uliimarisha kiwango chake cha ubadilishaji.

Kutokana na uthabiti wa shilingi ya Kenya, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA) imetangaza kupunguza bei ya mafuta kwa mwezi Julai hadi Agosti.

Dizeli itapungua kwa Sh1.50 kwa lita, na mafuta ya taa yatapungua kwa Sh1.30 kwa lita, na petroli kwa Sh1 kwa lita kusisitiza athari za nguvu za shilingi katika uthabiti wa bei ya mafuta.

Kufuatia ukaguzi huo, bei za mafuta jijini Nairobi zitakuwa Sh188.84 kwa lita moja ya super petrol, Ksh171.6 kwa lita ya dizeli na Sh161.75 kwa lita ya mafuta taa.

“Kuna dola zaidi kuliko mahitaji. Tuna sekta ya kilimo na pia tuna sekta ya utalii zilizoimarika,” alisema mfanyabiashara mmoja wa benki ya biashara.

Sekta ya kilimo ilichangia mapato ya dola kutokana na mauzo ya nje ya chai na kahawa. Wauzaji wa nje walipata kiasi kikubwa cha dola kutokana na mauzo ya mazao hayo.

Hii ilisababisha hitaji la shilingi huku wauzaji bidhaa nje wakibadilisha mapato yao ya dola kwa sarafu ya Kenya.

Shilingi imeimarika dhidi ya dola kwa muda wa miezi mitano iliyopita, faida ambayo ilitokana na hatua kali za sera za fedha za serikali.

Hata hivyo, kufikia Ijumaa wiki jana, ishara za kutimuliwa kwa Baraza la Mawaziri zilionekana kuwa na presha kwa Shilingi dhidi ya Dola huku ikidumisha uthabiti kwa sarafu za nchi za Afrika Mashariki.

Hatua zilizoleta utulivu wa sarafu ya humu nchini ni pamoja na ununuzi wa Sh310 bilioni (dola bilioni mbili) za Eurobond mwezi Februari na utoaji wa dhamana za Benki Kuu ya Kenya.

Benki ya Dunia iliorodhesha Shilingi ya Kenya kama sarafu inayofanya kazi vizuri zaidi katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Zaidi ya hayo, Benki Kuu ya Kenya katika Mkutano wake wa hivi majuzi wa Sera ya Fedha (MPC) ilifichua kuwa sarafu ya nchi hiyo iliongezeka kwa asilimia 17 dhidi ya sarafu nyingine za kimataifa.