Habari

SHOKA LA NYS: Wote wanaochunguzwa watumwa likizo ya lazima

May 21st, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

MAAFISA wote wanaochunguzwa kuhusiana na sakata ya ufisadi wa Sh9 bilioni katika Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), wamesimamishwa kazi ili kutoa nafasi kwa uchunguzi.

Hatua hiyo ilichukuliwa Jumapili na Waziri wa Utumishi wa Umma, Vijana na Jinsia, Prof Margaret Kobia (pichani) ambaye alisema maafisa hao ni walio katika idara za ununuzi na fedha katika shirika la NYS.

“Wote wanaochunguzwa wameagizwa kwenda kwa likizo ya lazima kuanzia sasa ili kuwezesha wapelelezi kukamilisha kazi yao bila kuingiliwa,” akasema Prof Kobia kwenye taarifa.

Hatua hii ilichukuliwa siku chache baada ya Katibu wa Wizara hiyo, Bi Lillian Mbogo-Omollo na Mkurugenzi Mkuu wa NYS, Bw Richard Ndubai kujiondoa mamlakani ili kutoa nafasi ya uchunguzi unaofanywa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).

Bi Omollo na Bw Ndubai leo wanatarajiwa kufika mbele ya Kamati ya Bunge inayosimamia Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC), ambayo inafanya uchunguzi wake huru kuhusu ufujaji wa fedha hizo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw Opiyo Wandayi, alisema safari hii ni lazima wahusika waadhibiwe kwani imekuwa kawaida maafisa wakuu wanaohusishwa na ufisadi kujiuzulu na baadaye hakuna anayeadhibiwa.

“Hii tabia ya kufuja pesa za umma lazima ikomeshwe. Ni lazima watu waadhibiwe kwa msingi wa mchango wao katika ufujaji wa mabilioni ya pesa,” akasema Bw Wandayi.

Wiki iliyopita, Prof Kobia alifika mbele ya kamati hiyo na akasema hawajakabidhiwa ripoti kamili ya upelelezi kutoka kwa DCI.

Kulingana na waziri huyo, ripoti ya mapema iliyowasilishwa kufikia sasa inahusu kupotea kwa Sh900 milioni, ingawa aliahidi wahusika wataadhibiwa mara tu ripoti kamili itakapotolewa.

 

Kampuni hewa

Ufichuzi uliofanywa na gazeti la Daily Nation ulionyesha kuna maafisa wa shirika hilo ambao waliunda kampuni hewa zilizotumiwa kufuja pesa kwa kuuzia NYS bidhaa na huduma hewa. Inaaminika kuna watu 40 ambao wanachunguzwa wakiwemo wakurugenzi wa kampuni ambazo zilifanya biashara na NYS kwa njia zisizoeleweka.

Sakata hii imefufua upya mijadala kuhusu kujitolea kwa serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kupambana na ufisadi tangu walipoingia mamlakani 2013.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, rais alirejelea kusema atapambana vikali na janga hilo linalotajirisha watu wachache.

Hata hivyo, wananchi wengi kwenye mitandao ya kijamii walitilia shaka kama kutakuwa na mabadiliko wakati huu wakisema ni kawaida kwa maafisa wakuu kujiuzulu wakati wanapohusishwa na ufisadi, na rais kutangaza hatua kali dhidi ya wanaohusika kwa ufisadi, lakini hakuna anayeadhibiwa baadaye.