Hisia mseto baada ya Wazee wa Agikuyu kumtembelea Raila, Bondo
NA WAANDISHI WETU
BARAZA la Wazee wa Jamii ya Agikuyu limekana madai kuwa limemwidhinisha kiongozi wa ODM Raila Odinga kama mgombeaji wa urais 2022, siku moja baada kumtembelea nyumbani kwake, Bondo, Kaunti ya Siaya.
Mkutano huo na kauli ya kiongozi wa wazee hao Wachira Kiago kwamba jamii hiyo inasimama na Bw Odinga umeibua hisia mseto miongoni mwa wanachama wa makundi mengine ya kijamii.
Makundi hayo yametaja ziara hiyo kama “isiyo na maana yoyote.”Lakini jana Mzee Kiago alijitokeza na kufafanua kuwa hawakumwidhinisha Bw Odinga kwa urais wakati wa mkutano huo.
“Hatukupeleka ajenda ya kisiasa katika mkutano huo. Tulilenga kujenga ushirikiano wa amani kati ya jamii zetu. Hatukuidhinisha mtu yeyote,” Bw Kiago akaambia Taifa Leo.
Japo baraza hilo la wazee halikutoa msimamo wake kuhusu suala hilo, mkutano huo ulitoa dhana kuwa jamii ya Agikuyu inamuunga mkono Bw Odinga kuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta.
Kundi kwa jina Kiama Kia Ma, kitengo cha kitamaduni cha baraza hilo, kimepuuzilia mbali kundi linaloongozwa na Mzee Kiago likisema sio halali.
“Hao sio wanachama halali wa baraza la wazee la jamii ya Agikuyu na hawawakilishi watu wa jamii hiyo. Wakati mwaka ukijiri jamii hii itatangaza msimamo wake,” mwenyekiti mwenza wa kundi la Kiama Kia Ma Kigochi Waimiri akasema.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Wambugu Nyamu pia alipuuzi;ia mbali mkutano huo akisema haitamwezesha Bw Odinga kupata ufuasi katika eneo la Mlima Kenya.
“Mkutano huo ulikuwa ni wa baraza la wazee pekee wala sio watu wa jamii ya Agikuyu. Wazee hao hawakushirikisha mtu yeyote na hivyo msimamo wao hauwakilishi ule wa watu wote,” akasema Bw Nyamu.
Wabunge wa mrengo wa Tangatanga pia walipuuzilia mbali ziara ya Wazee hao Bondo wakiitaja kama ‘ya kitalii’.
Wakati huo huo wazee wa jamii ya Ameru, maarufu kama Njuri Ncheke wamejitenga na wazee waliomtembelea Bw Odinga nyumbani kwake, Bondo, wakisema hawakushauri kuhusu suala hilo.
Katibu Mkuu wa baraza hilo Josphat Murangiri alisema Mzee Kiago na wenzake hawakujadili suala hilo na viongozi wengine katika eneo la Mlima Kenya.
Na MWANGI MUIRURI, NICHOLAS KOMU NA GITONGA MARETE