HabariMakala

SYSTEM YA MADENI: Rotich alivyokopa kiholela

September 8th, 2018 3 min read

Na CHARLES WASONGA

KUPANDA kwa madeni ya Kenya kutoka Sh1.77 trilioni mnamo 2013 hadi Sh5.1 trilioni mwaka huu, ndio chanzo cha masaibu yanayowazonga Wakenya ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta, kwa mujibu wa wataalamu.

Wachanganuzi wanasema hali mbaya ya kiuchumi nchini inachangiwa na tamaa ya kukopa fedha nyingi, haswa kutoka China, mikopo ambayo ni ya kibiashara na hivyo kutozwa riba ya juu zaidi.

Kwa mfano, inakadiriwa kuwa Sh337 bilioni ambazo Kenya ilikopa kutoka China kufadhili awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) zitalipiwa riba ya kima cha Sh82.85 bilioni kila mwaka kuanzia Julai mwaka ujao kutoka Sh38.5 bilioni mwaka huu.

Hofu kuhusu mzigo wa madeni ya Kenya inatokana na kupanda kwake kwa kasi kuliko kiwango cha mapato ya serikali, na hivyo kupunguza uwezo wake kulipa.

Kimsingi, uwezo wa taifa kulipa madeni yake hutegemea pakubwa uwezo wake wa uzalishaji na kuimarisha ukusanyaji wa mapato yake.

Kwa mfano, Kenya ilikosa kukusanya mapato ya kima cha takriban Sh500 bilioni katika mwaka wa kifedha uliopita wa 2017/2018, hali iliyoilazimu serikali kukopa kutoka nchini na nje kuziba pengo hilo.

 

Hofu

Kwa hivyo, wataalamu wa masuala ya uchumi wanaonya kuwa, hamu ya Kenya kuchukua mikopo ya kibiashara huenda ikachangia kushindwa kwake kulipa madeni yake.

“Kimsingi, Kenya inafaa kuwa ikichukua mikopo yenye riba ya chini, lakini hatujaweza kuafikia lengo hili katika siku za hivi karibuni,” akasema John Mutua afisa wa mipango katika Taasisi ya Masuala ya Uchumi (IEA).

Kuanzia mwaka jana, serikali imekuwa ikishauriwa kupunguza hamu ya kuchukua mikopo, lakini kufikia sasa ushauri huo umepuuzwa.

Shirika la Fedha Ulimwenguni

“Tumeishauri serikali kuanzisha mchakato wa kupunguza madeni yake,” mwakilishi wa Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) nchini Jan Mikkelsen aliambia Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti Februari mwaka huu.

Lakini maafisa wakuu serikalini, wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, wamepuuza tahadhari hizo wakishikilia kuwa uchumi ni thabiti na unaweza kustahimili mzigo wa madeni.

“Ningetaka kuwahakikishia Wakenya kwamba hakuna wakati ambapo serikali itashindwa kulipa madeni yake,” Rais Kenya akasema kwenye Hotuba kuhusu Hali ya Taifa aliyotoa Bungeni Machi 26, mwaka huu.

Kinyume na utawala wa Rais mstaafu Mwai Kibaki ambaye alihimiza mfumo thabiti wa ukusanyaji ushuru na kupunguza mikopo, serikali ya Jubilee imeacha mianya mikubwa ya kukwepa ushuru huku ikionekana kutekwa na mikopo ya nje.

Wadadisi sasa wanasema wa kulaumiwa kwa mzigo huu wa madeni ni Waziri wa Fedha Henry Rotich, na maafisa wakuu katika wizara yake.

 

Kinaya

Ni kinaya kuwa Wizara ya Fedha imeshindwa kusimamia mzigo wa madeni ilhali ina maafisa wenye tajriba pana. Watu ambao wamewahi kushikilia nyadhifa za juu katika Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF).

Wao ni katibu Dkt. Kamau Thugge ambaye amewahi kuhudumu kama mtaalamu wa masuala ya uchumi katika IMF kwa muda wa miaka 21.

Naye Dkt Geoffrey N. Mwau, pia aliwahi kuhudumu katika shirika la IMF kama mshauri wa masuala ya uchumi aliyesimamia Rwanda, Malawi, Botswana na Uganda huku Mutua Kilaka akihudumu kama Katibu wa Usimamizi katika Wizara tangu 1975.

Umeme mashinani

“Inashangaza kuwa Rotich amefeli kushauri wakuu wake kwamba matatizo yanaisibu nchi hii wakati huu yanachangiwa na ukopaji kupita kiasi. Kwa mfano, kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, serikali, chini ya usimamizi wa Rotich, imekopa kitita cha Sh3.4 trilioni,” anasema mhadhiri wa masuala ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Nairobi Samuel Nyandemo.

“Rotich amegeuka kuwa mtu wa kusema “Ndio” kwa wakubwa wake Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto, wanapomtaka kutia saini mikataba ya mikopo ya kufadhili miradi mikubwa ya kisiasa kama SGR na usambazaji umeme mashinani,” anaeleza.

Ni kutokana na haja ya kulipa madeni hayo, anafafanua, ambapo Wizara ya Fedha sasa imeamua kuwaumiza Wakenya masikini kwa kupandisha ushuru kwa bidhaa na huduma za kimsingi, kama vile, mafuta na huduma za mawasiliano ya simu ya mkono,” anaongeza msomi huyo.

 

Sifa mbaya

Naye Waziri wa zamani wa Fedha, Musalia Mudavadi anasema Rotich amejizolea sifa mbaya kama Waziri wa Fedha ambaye aliiwekea Wakenya mzigo mkubwa ambao umewasababishia madhara mengi.

“Rotich anafaa kujiuliza ni kwa nini madeni yamepanda ilhali manufaa ya zaidi ya Sh3 trilioni alizokopa hayaonekani.

Ama kwa hakika atakumbukwa kama Waziri wa Fedha aliyetumbukiza Kenya katika lindi la masaibu mengi zaidi kuliko watangulizi wake, nikiwemo,” Mudavadi ambaye ni kiongozi wa chama cha ANC alisema juzi alipohojiwa kwenye studio za runinga ya KTN.

Watangulizi wengine wa Rotich ni; James Gichuru, Kibaki, Arthur Magugu, George Saitoti, Simeon Nyachae, Francis Masakhalia, Chris Okemo, Chris Obure, David Mwiraria, Amos Kimunya, John Michuki, Uhuru Kenyatta na Njeru Githae ambao hawakuitumbukiza nchi katika katika matatizo ya kiuchumi kiasi hiki.

Hali hii ndio imepelekea Mbunge wa Emgwen Alex Kosgei kupendekeza mswada wa kudhibiti kiwango cha fedha ambazo serikali inapaswa kukopa katika kipindi fulani.

Wizara ya Fedha nayo imeanzisha mchakato wa kubuni kundi la watalaamu watakaoratibu mbinu za kuiwezesha Kenya kusimamia mikopo yake.