• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Barabara hatari eneo la Ngunguru-Karatina

Barabara hatari eneo la Ngunguru-Karatina

Na SAMMY WAWERU

WAKAZI wa kijiji cha Ngunguru, eneo la Gathogorero, Karatina Kaunti ya Nyeri wanalalamikia barabara hatari inayoendelea kuwahangaisha. 

Barabara ya Karatina – Mukurweini, katika eneo la Ngunguru, wenyeji wanateta haina matuta wala alama za barabara kutahadharisha madereva kupunguza kasi ya magari.

Shule ya Msingi ya Gathogorero i karibu mita 200 kutoka barabara hiyo.

“Tumepoteza watoto kadha wakivuka barabara wakati wakienda au kutoka shuleni. Majuzi, wawili wamepigwa dafrau na gari na kufariki,” mmoja wa wakazi akaambia  Taifa Leo kwenye mahojiano.

Kulingana na mwenyeji huyo, si mara moja, mbili au tatu wamelalamikia kuhusu usalama wa barabara hiyo.

Kufuatia ziara yetu, tulithibitisha eneo hilo halina alama za barabara wala ilani kuelekeza madereva.

Isitoshe, magari yalionekana kuendeshwa kwa mwendo wa kasi, jambo ambalo linazua usalama wa wakazi, hasa wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Gathogorero.

“Awali, walimu walikuwa wakisaidia watoto wetu kuvuka ila sasa hatuwaoni,” akalalamika mkazi mwingine. 

Kwa mujibu wa sheria za trafiki, barabara iliyoko katika mazingira yenye shule inapaswa kuwa na vibango kuelekeza madereva kupunguza kasi ya magari. 

Hali kadhalika, inapaswa kuwa na matuta au vivukio maalum kwa wanaotembea kwa miguu – vivukomilia. 

You can share this post!

Kocha Nuno Espirito Santo kuvunja ndoa kati yake na Wolves...

Barcelona yampa Lionel Messi likizo ya mapema kujiandaa kwa...