• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Madaktari 10 wa Mombasa kufaidika kwa mafunzo zaidi nchini Uturuki kwa juhudi za Shahbal

Madaktari 10 wa Mombasa kufaidika kwa mafunzo zaidi nchini Uturuki kwa juhudi za Shahbal

WACHIRA MWANGI na CHARLES WASONGA

MFANYABIASHARA wa Mombasa Suleiman Shahbal amefaulu kupata nafasi zitakazowawezesha madaktari 10 kutoka kaunti hiyo kupokea mafunzo zaidi nchini Uturuki.

Bw Shahbal alisema amepata nafasi zitakazowawezesha madaktari hao kupokea mafunzo kuhusu mbinu za kutibu kansa katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Medeniyat kilichoko jijini Instanbul.

Bw Shahbal ambaye pia amejitosa katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Mombasa, alisema hayo baada ya kukutana na Naibu Chansela wa Chuo hicho Profesa Sadrettin Pence.

Msomi huyo ndiye msimamizi wa huduma za kimatibabu nchini Uturuki.

“Profesa Pence amejitolea kuwapa mafunzo madaktari 10 katika tiba ya kansa, bila malipo, katika hospitali ya chuo hicho kikuu. Hospitali hiyo ndiyo kubwa zaidi nchini Uturuki. Nitawasilisha nafasi hiyo kwa Serikali ya kaunti ya Mombasa. Madaktari wanaotaka mafunzo hayo wanashauriwa kuwasiliana na afisi yetu kwa maelezo zaidi. Kuna mengi yanayoweza kufanywa kwa ushirikiano na Uturuki ili kutusaidia hapa Mombasa,” Bw Shahbal akasema kwenye ujumbe katika ukurasa wake wa Facebook.

Profesa Pence na Bw Shahbal walikutana Jumapili nchini Uturuki ambako mfanyabiashara huyo alikuwa amealikwa kwa mikutano na wawekezaji.

Alisema wawekezaji hao wataisaidia pakubwa Kaunti ya Mombasa ikiwa atachaguliwa kuwa Gavana katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Bw Shahbal alisema Profesa Pence, ambaye amewahi kuanzisha hospitali katika nchi za Sudan, Somalia miongoni mwa nyingine, amekubali kuanzisha hospitali kadha katika Kaunti ya Mombasa.

You can share this post!

AFCON: Wanahabari watatu wa Algeria wavamiwa na wahalifu...

AFCON: Gabon wazamisha limbukeni Comoros katika Kundi C

T L