• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:55 AM
Uganda Airlines yalenga kuongeza safari zake Mombasa

Uganda Airlines yalenga kuongeza safari zake Mombasa

NA FARHIYA HUSSEIN

SHIRIKA la ndege la Uganda Airlines limejipanga kuongeza safari zake za moja kwa moja kati ya Entebbe na Mombasa baada ya Kenya kuidhinisha kufunguliwa kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mombasa kwa mashirika ya ndege ya kigeni.

Shirika hilo la ndege, ambalo lilianzisha safari za moja kwa moja hadi jijini Mombasa mwaka wa 2019 likiwa na lengo la kuwa na abiria 76, kwa sasa husafiri hadi jijini humo mara tatu kwa wiki. Siku hizo ni Jumatatu, Ijumaa na Jumapili.

Likilenga kujiimarisha, shirika hilo linataka kufufua sifa yake ya safari za ndege huku kukiwa na ushindani mkali kutoka kwa mashirika ya ndege ya kimataifa kama vile Fly Dubai, ambalo ndege zake zinafanya safari zake mara nne kwa wiki hadi Mombasa.

Meneja wa Shirika la Ndege la Uganda nchini Kenya, Bi Peggy Macharia, alibainisha kuwa shirika hilo la ndege linanuia kuitangaza Mombasa kama eneo la shughuli za biashara na wala sio tu sehemu ya utalii.

“Katika miaka minne ambayo ndege zetu zimesafiri Mombasa, tumeona ukuaji mkubwa hata baada ya janga la Covid-19. Tuna wateja wetu wengi kutoka Uganda ambao hutembelea mji wa kitalii kwa biashara,” alisema Bi Macharia, akiongeza kuwa walilazimika kuhamisha ofisi zao za Mombasa na kusogea karibu na wateja wao, ambapo anabainisha kuwa hatua hiyo imeongeza wateja zaidi.

“Ofisi zetu zilikuwa Nyali, lakini tuliona ni vyema tukihamia mjini karibu na abiria, ambako kuna watu wengi. Tulikuwa tumepokea malalamiko kuhusu umbali wa ofizi zetu. Hii ni sehemu moja ambayo tumeona katika ukuaji wa uchumi na biashara. Tunatumai kuongeza idadi ya wateja wetu. Tumeona biashara nyingi kutoka Uganda zikija bandarini na Wakenya wakienda Uganda kama watalii,” alisema Bi Macharia.

Shirika hilo la ndege linasema safari za saa moja na dakika 50 zinalenga watalii na wafanyabiashara wa Uganda ambao wanategemea bandari ya Mombasa kufanya biashara kwa vile bidhaa nyingi zinazoagizwa nchini hupitia bandari hiyo.

Serikali mwezi huu wa Agosti iliidhinisha ndege za mashirika ya kigeni kuruka moja kwa moja hadi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi jijini Mombasa, na kuahidi upanuzi katika sekta ya utalii, ambayo ni tegemeo la kiuchumi eneo hilo.

Kufuatia hatua hiyo, ndege za shirika la Ethiopian Airlines huruka moja kwa moja hadi Mombasa mara mbili kwa wiki.

Mashirika mengine kama vile Turkish Airlines yanaendelea kutathminiwa.

Akizungumza jijini Mombasa wakati wa mashindano ya gofu, Mwakilishi wa Bodi ya Utalii ya Uganda katika Soko la Afrika Bw Anthony Ochieng alisema mwaka 2022, takriban Wakenya 400,000 walitembelea Uganda kama watalii, wasafiri wa shughuli za kibiashara, na wengine wenye uhusiano wa kitamaduni na kifamilia.

“Jumla ya wachezaji 200 wa mchezo wa gofu kwa sasa wanashiriki mashindano hayo, na lengo kuu ni kuhakikisha tunashirikiana kwa karibu zaidi na mashirika ya safari za ndege hapa Mombasa na nchini Uganda, na mojawapo ya mashirika hayo ni Uganda Airlines. Wakenya wengi wanapenda utalii na burudani, na jiji la Kampala bila shaka ni kitovu cha majukwaa ya burudani Afrika Mashariki,” alisema Bw Ochieng.

Bw Ochieng alibainisha kwamba mwaka 2022, washiriki 100 wa biashara za usafiri wa kutoka nchini Uganda walihudhuria kongamano la utalii lililofanyika katika hoteli ya Pride Inn.

Nao Wakenya 50 wa biashara ya usafiri walitembelea Uganda kwa safari ya starehe.

Bw Ochieng anabainisha kuwa wanalenga kupanua safari katika viwanja vingine vya ndege vya pwani siku zijazo.

“Diani ni eneo tunalopenda. Raia wengi wa Uganda huzuru Pwani haswa Diani, kwa harusi, karamu, likizo na fungate, miongoni mwa sababu nyingine,” alisema Bw Ochieng.

Shirika la Ndege la Uganda lilianzishwa wakati wa utawala wa Rais wa zamani wa Uganda Idi Amin mwaka wa 1976, lakini shirika hilo lilifutiliwa mbali mwaka 2001 baada ya kushindwa kwa jitihada za kubinafsisha kampuni hiyo iliyotawaliwa na ufisadi na usimamizi mbovu kipindi hicho.

Ndege za shirika hilo husafiri katika nchi 11 za Afrika, ikiwa ni pamoja na Tanzania katika maeneo matatu, Burundi, Sudan Kusini, Afrika Kusini, na safari ijayo nchini Nigeria ndani ya miezi michache.

  • Tags

You can share this post!

Wafanyabiashara waomba taa irekebishwe sokoni Kisekini

Namuomba Mungu wa mwisho awe ni wewe – Hamisa Mobetto

T L