Afya na Jamii

Tahadhari wanaougua saratani ya uume wakiendelea kuongezeka

Na CECIL ODONGO July 22nd, 2024 1 min read

IDADI ya watu wanaougua saratani ya uume inaendelea kupanda kote ulimwenguni kutokana na utafiti na uchunguzi uliofanywa na wataalamu.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sun Yat-Sen nchini China, wanaume ambao wanaugua kansa ya uume wanatarajiwa kupanda kwa asilimia 77 kwa muda wa miaka 26 ijayo. Utafiti ulioendeshwa na chuo hicho, ulishirikisha mataifa 43 kutoka mabara mbalimbali ya ulimwenguni. Mataifa ambayo kansa hiyo imekuwa ikienea sana ni yale ya bara Ulaya.

“Ingawa mataifa yanayoendelea bado yana vifo vingi vinavyotokana na kansa ya uume, visa vingi sana vinatokea katika mataifa ya Bara Ulaya,” utafiti huo unaeleza.

Ujerumani, Uingereza na Brazil ni kati ya nchi ambapo saratani ya uume imepanda mno. Kati ya dalili za kansa ya uume ni kubadilika kwa rangi ya uume, vitu vya majimaji kuanza kutoka ndani ya uume na pia mabadiliko kuhusu hamu ya ngono.

“Sababu nyingine zinazosababisha kansa ya uume ni kushiriki ngono bila kutumia kinga, uume kuwa mchafu na pia wanaume ambao hawajatahiriwa wako katika hatari ya kupatwa na ugonjwa huo,” akasema Dkt Neil Barber ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya kuambukizana.

Aidha, watafiti walibaini kuwa ugonjwa huo hasa upo miongoni mwa wanaume ambao wana umri wa miaka 60 au zaidi. Japo visa vya wale ambao wana kansa hii vinaendelea kupanda, wanaume hawafai kuingiwa sana na wasiwasi kwa sababu ni kati ya kansa ambayo ni nadra sana kupatikana kwao ikilinganishwa na jinsia nyingine. Ulimwenguni, Uganda ambao ni majirani wa Kenya wana visa vingi vya wanaougua kansa ya uume huku wakifuatwa na Brazil.

Nchini Uganda kati ya 2008 na 2012 wanaume 220 walipatikana na kansa ya uume kati ya wanaume 100,000 nao nchini Brazil, ni wanaume 210 saratani kati ya wanaume 100,000 katika kipindi hicho.