Michezo

Tumevunjika moyo sana, wasema Uingereza wakipoteza taji la Euro kwa mara nyingine

Na MASHIRIKA July 15th, 2024 2 min read

BAADA ya miaka minane kama kocha wa Uingereza, Gareth Southgate huenda akafunganya virago na kuondoka baada ya kupoteza 2-1 dhidi ya Uhispania katika fainali ya mashindano ya Euro 2024 ambayo yalikamilika Jumapili usiku katika Uwanja wa Olimpiki nchini Ujerumani.

Wengi walipigia upatu Uhispania kutwaa kombe hilo kwani kikosi cha Luis de la Fuente kiliimarika kuanzia mwanzoni mwa mashindano hadi mwisho.

Katika mechi za hatua ya makundi, waliongoza Kundi B kwa alama tisa bila kupoteza mechi yoyote.

Uingereza kwa upande mwingine, walisuasua katika Kundi C wakiongoza kwa alama tano. Walipata ushindi mara moja na kutoka sare mara mbili.

Mshambuliaji Nico Williams aliwashangaza Uingereza kwa kufunga bao la ufunguzi dakika ya 47 kabla ya Uingereza kusawazisha kupitia nguvu mpya Cole Palmer dakika ya 73.

Mshambuliaji Mikel Oyarzabal alifungia Uhispania bao la ushindi dakika ya 86.

Southgate sasa ndiye kocha pekee ambaye amepoteza katika fainali mara mbili katika mashindano ya Euro.

“Sioni ni wakati mzuri wa kuamua mambo ya kukaa kwangu kwenye usukani. Nahitaji kufanya mazungumzo hayo na wahusika wa shirikisho la taifa la soka mwanzo. Sitazungumzia hayo hadharani kwanza,” alisema South Gate baada ya mechi hiyo.

Naye nahodha Harry Kane alituma barua ya huzuni kwa mashabiki wa Uiingereza; “Tumevunjika moyo kwamba hatukufanikiwa kufikia lengo letu. Ilikuwa michuano mirefu na migumu sana na ninajivunia sana wachezaji wenzangu pamoja na benchi ya kiufundi kufika fainali. Hata hivyo, tulikosa ubingwa na tutalazimika kujikusanya tena, kujipigapiga vimbi na kuwa tayari kupigana tena katika jezi ya Uingereza. Asanteni kwa mashabiki wote waliotuamini na kutuunga mkono hadi mwisho kabisa!”

Ikiwa Southgate ataondoka, ataondoka na kuacha historia katika timu hiyo ikilinganishwa na walivyokuwa mwaka 2016 kurudi nyuma chini ya kocha Sam Allardyce.

Gareth aliingia usukani na kumpa kila mtu tabasamu – kuunganisha kikosi, kukifikisha nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na kisha fainali ya Mashindano ya Ulaya mwaka 2021, na kikosi kidogo kuliko alicho nacho wakati huu.

Kwa kufanikisha mambo hayo yote, anastahili heshima kubwa na shukrani, lakini ni jambo la kusikitisha kwamba – kwa kazi yake nzuri yote – Gareth hakufanikiwa kabisa kuibwaga Uhispania katika fainali.

Ikiwa ataondoka, basi ameweka timu katika nafasi nzuri sana kwa mtu mwingine kuchukua hatamu, kuendeleza timu mbele na kushinda mashindano makubwa.

Kwanza, Uhispania walitawala mchezo. Lamine Yamal alifikisha miaka 17 siku ya Jumamosi. Jumapili jioni, alisherehekea kwa kusaidia Uhispania kushinda Ubingwa wa Ulaya.

“Ni zawadi bora ya kuzaliwa,” alisema winga huyo baada ya kutangazwa Mchezaji Mchanga kabisa wa Mashindano na kisha kuinua kombe la Henri Delaunay.

“Lamine ni mchezaji wa kipekee,” mchezaji mwenzake Nico Williams aliongeza.

Yeye ndiye mchezaji mchanga zaidi kufika katika fainali za Euro au Kombe la Dunia. Alichangia katika ufungaji wa bao la Williams lilimwezesha kumaliza mashindano kwa kusuka mabao manne – mara mbili zaidi ya mchezaji mwingine yeyote.

Wachezaji wengi maarufu hawakuridhisha sana Ujerumani, lakini Yamal aliwazidi matarajio wote.