HabariHabari za KitaifaSiasa

Ufichuzi: Hawa ndio walisuka ndoa ya Ruto na Raila

Na MOSES NYAMORI August 5th, 2024 2 min read

WANDANI wakuu wa kinara wa upinzani Raila Odinga waliohusika katika makubaliano na Rais William Ruto, walifanya msururu wa mikutano usiku kabla ya rais kutangaza hadharani majina ya mawaziri wateule, Taifa Leo imebaini.

Kakaye mkubwa Odinga, Oburu Oginga, aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju, Kiranja wa Wachache Bungeni Junet Mohamed, Bw Joe Ager na Profesa Adams Oloo walishiriki mazungumzo yaliyoishia katika uteuzi wa viongozi wa ODM serikalini.

Bw Mohamed pia alitekeleza wajibu mkubwa katika muafaka kati ya Bw Odinga na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo pia alihudumu kama mjumbe wa Bw Odinga katika harakati za kuafikia makubaliano hayo na Rais Ruto.

Bw Obasanjo alikuwa nchini siku chache kabla ya Rais kutaja majina ya watu aliowapendekeza kuhudumu katika baraza lake jipya la mawaziri.

Kwa upande mwingine, Dkt Ruto aliwakilishwa na kundi dogo lililoshirikisha kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichung’wah na mwenzake wa Seneti Aaron Cheruiyot, katika mchakato huo. 

Vikao vya usiku

Wahusika kadhaa tuliozungumza nao walifichua kuwa mikutano mingi ilifanyika usiku katika mkahawa wa Entim Sidai, Karen unaomilikiwa na Bw Tuju ilhali mingine ilifanyika katika afisi za Wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga (JOOF).

Bw Tuju alithibitisha kukutana na baadhi ya watu waliohusika katika mazungumzo hayo. Alisema kuwa yeye ni mwanachama wa Jubilee na hivyo hawezi kushiriki mapatano kwa niaba ya ODM.

Bw Tuju pia alithibitisha kuwa alihudhuria mkutano mmoja katika SKM Centre siku moja baada ya Rais Ruto kuwateua mwenyekiti wa ODM John Mbadi, Kiongozi wa Wachache Opiyo Wandayi, Wycliffe Oparanya na Hassan Joho kuwa mawaziri wateule.

“Ni kweli nilikuwa huko asubuhi. Oparanya, Jeremiah Kioni, Peter Munya na Kalonzo Musyoka pia walikuwepo katika mkutano huo,” akasema Bw Tuju. 

Kalonzo alikataa wito

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bw Kioni alifichua maelezo kuhusu mkutano huo wa Julai 25, 2024. Alisema Tuju alijaribu kumshawishi Bw Musyoka kuunga mkono makubaliano kati ya Rais Ruto na Bw Odinga.

Bw Oparanya, Kioni akasema, aliwafichulia waliohudhuria mkutano huo kwamba alitengewa nafasi katika baraza la mawaziri.

“Lakini tulimshauri kwamba akatae nafasi hiyo kwa sababu hii ni serikali iliyokuwa ikiendelea kuporomoka,” Bw Kioni akaeleza.

Lakini wandani wa Bw Odinga walishawishika kuwa taifa lingepoteza zaidi endapo serikali ya Rais Ruto ingeporomoka. Hii ni baada ya kuibuka uvumi kwamba baadhi ya viongozi wa Azimio walikuwa wameanzisha mazungumzo na Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa lengo la kubuni muungano kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Aidha, serikali ya Ruto ilikuwa ikizongwa na shinikizo kutoka kwa vijana wa Gen Z.