Habari za Kitaifa

Ukatili wa polisi wadhihirika tena kwenye maandamano licha ya kukemewa vikali

Na WAANDISHI WETU July 17th, 2024 1 min read

WATU kadhaa waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi waliotumia nguvu kupitia kiasi kukabili waandamanaji wasiokuwa na silaha.

Vijana wawili waliangamizwa kwa risasi mjini Kitengela, Kaunti ya Kajiado na wawili mjini Kibwezi, Kaunti ya Makueni.

Kufikia wakati wa kupeperusha ripoti hii, habari za watu zaidi kufyatuliwa risasi na maafisa wa polisi wakiandamana zilikuwa zikiripotiwa maeneo tofauti nchini.

Baadhi ya waliojeruhi kwa risasi, mikebe ya vitoa machozi ni watetezi wa haki za binadamu, wanahabari na watoto.

Mjini Nakuru, mwanahabari wa Media Max (K24), Catherine Wanjeri alijeruhiwa kwa risasi na maafisa wa polisi akifuatilia maandamano.

Alikimbizwa upesi na wenzake kupokea matibabu katika hospitali moja ya Nakuru.

Katikati ya jiji, mtoto mvulana alijeruhiwa mguuni huku wazazi wake wakitoroka polisi walipofyatua vitoa machozi kiholela.

Katika Kaunti ya Kisumu, mtetezi wa Haki za Kibinadamu Boniface Akach alipigwa kifuani na mkebe wa gesi ya kutoa machozi akishiriki maandamano.

Mwandamanaji mwingine alipigwa risasi kichwani na kukimbizwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga.

Bw Akach aliambia Taifa Leo kwamba, alikuwa akizungumza polisi walipomgeukia na kumjeruhi.

“Nilikuwa nikizungumza nao na ghafla wakawa na chuki na mmoja wao akanielekezea bunduki yake na kufyatua mkebe kwa karibu sana,” akasema Bw Akach.

Alikimbizwa hospitali kwa pikipiki.

Katika mji wa Homa Bay, makundi mawili ya vijana yalikabiliana wakati wa maandamano ya kuipinga serikali.

Wakati huo huo, hali ya wasiwasi ilikumba mji wa Siaya, na kuwalazimu wamiliki wa biashara kufunga maduka yao.

Ripoti za Stanley Ngotho, Pius Maundu, Steve Otieno, Rushdie Oudia, George Odiwuor na Kassim Adinasi