Habari za Kitaifa

Urafiki kati ya Raila na Uhuru wayeyuka

Na BENSON MATHEKA August 25th, 2024 2 min read

MNAMO Julai 23 2023, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alimtaja kiongozi wa ODM Raila Odinga kama rafiki yake ambaye Serikali ya Rais William Ruto haikutaka azungumze naye.

Hii ilikuwa kilele cha maandamano yaliyoitishwa na upinzani dhidi ya Serikali ya Kenya Kwanza iliyomlaumu Uhuru kwa kuyafadhili.

“Kwani siruhusiwi kuzungumza na marafiki wangu?” Uhuru alisema akilaumu polisi kwa kumlenga walipovamia nyumba ya mwanawe kwa dai alimiliki silaha kinyume cha sheria.“Serikali hii inataka nini?” alihoji.

Mwaka mmoja baadaye jibu linaonekana kudhihirika huku Rais Ruto akionekana kumvuta Odinga upande wake na kumtenganisha na Uhuru.

Ni Uhuru aliyechangia kuundwa kwa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kwa kushawishi vyama vya kisiasa kuungana ili Odinga apate chombo cha kutumia kugombea uchaguzi mkuu wa 2022 dhidi ya Ruto ambaye alikuwa naibu rais.

Baada ya Ruto kuanza usuhuba wa kisiasa na Odinga mwishoni mwa mwaka wa 2023, waziri mkuu huyo wa zamani anaonekana kujitenga na Uhuru huku chama chake cha ODM kikimlaumu rais huyo mstaafu kwa kupanga mapinduzi katika muungano wa upinzani.

Wiki hii, chama hicho kilisusia mkutano ambao Uhuru aliitisha kujadili mustakabali wa Azimio baada ya ODM kuchangamkia serikali.

Japo vinara wenza wa Azimio walisema ODM ilikuwa imealikwa katika mkutano huo, mwenyekiti wake Gladys Wanga alisema hawakuwa na habari na wasingehudhuria kwa kuwa Uhuru hana mamlaka ya kuuitisha.

“Hatuna habari kuhusu mkutano wowote na kiongozi wa chama chetu Raila Amolo Odinga ndiye kiongozi wa Azimio. Mkutano wowote unapaswa kupangwa na ODM,” alisema na kuongeza ni Katibu Mkuu wa Azimio, Junet Mohamed, mshirika wa Raila anayepaswa kuitisha mkutano kama huo.

Uhuru ni mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio. Chama hicho kilihofia kuwa Uhuru alinuia kumbandua Raila kama kiongozi wa Azimio kufuatia ukuruba wa ODM na serikali.

Wachanganuzi wa siasa wanasema inaonekana Ruto amefaulu kumvuta Raila kutoka mrengo wa Uhuru kurejesha ushirika waliokuwa nao kuelekea uchaguzi mkuu wa 2007.

“Kila dalili zinaonyesha ushirikiano wa Raila na Uhuru umeingia doa na ameruka upande wa Ruto. Ni Ruto ambaye amefaulu kumaliza urafiki wa kisiasa kati ya Raila na Uhuru na kwa kufanya hivyo akarejesha ushirikiano wake na Raila wa mwaka wa 2007,” asema mchambuzi wa siasa George Kimani.

Uhuru hakugombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2007 ambao aliamua kumuunga Mwai Kibaki aliyekuwa akitetea kiti chake akishindana na Raila ambaye alikuwa akiungwa mkono na Ruto na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi katika chama cha ODM.

Katika uchaguzi mkuu wa 2013, Ruto na Uhuru waliungana kupitia muungano wa Jubilee dhidi ya Raila aliyekuwa akiungwa mkono na Kalonzo Musyoka kama mgombea mwenza wake na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula katika muungano wa Cord.

Ruto na Uhuru walishinda na katika muhula wao wa pili wakakosana na Uhuru akachangamkia Raila ambaye alimuunga katika uchaguzi mkuu wa 2022 dhidi ya Ruto.

Baada ya Ruto kuingia mamlakani, ushirika wa Uhuru na Raila sasa unaonekana kuyeyuka kiongozi huyo wa ODM akimchangamkia Ruto katika kile ambacho wadadisi wanasema ni karata ya kisiasa.

Japo Raila alisema ni Uhuru aliyemtuma kwa Ruto kutuliza nchi kufuatia maandamano ya vijana yaliyotikisa serikali, wadadisi wanasema ni kiongozi wa nchi aliyefaulu kuvunja ushirika waliokuwa nao dhidi yake uchaguzi uliopita.

Inasemeka kuwa Uhuru hakuchangamkia azma ya Raila kugombea uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) na usuhuba wake na Ruto.

Bw Kimani anasema ikiwa ni kweli Uhuru alijaribu kumshawishi Raila asiendee wadhifa huo, basi amegeuka hasimu wa Ruto na Raila.