Habari za Kaunti

Viongozi walumbania chuo kikuu Ruto akizuru Nyamira

Na RUTH MBULA August 12th, 2024 2 min read

WANASIASA wa Nyamira wametofautiana kuhusu mahali ambapo chuo kikuu kinastahili kuanzishwa katika kaunti hiyo huku Rais William Ruto akianza ziara ya siku tatu eneo la Gusii leo.

Mbunge wa Mugirango Joash Nyamoko amesema jiwe la msingi la ujenzi wa chuo hicho litawekwa na Rais katika Shule ya Upili ya Kiabonyoru.

Hata hivyo, mwenzake wa Mugirango Mashariki Stephen Mogaka amesema suala la kuzinduliwa kwa ujenzi wa chuo hicho halipo katika shajara ya Rais.

Kando na wanasiasa hao wawili, Gavana Amos Nyaribo, wabunge Patrick Osero (Borabu) na Clive Gisairo wa Kitutu Masaba pia wapo katika mzozo huo kuhusu mahali pa ujenzi wa chuo hicho kipya.

Aidha, kuna mapendekezo mengine kuwa chuo hicho kinastahili kujengwa Manga katika eneobunge la Kitutu Masaba na shule za upili za Kebaso na Riakimai (Mugirango Magharibi).

Pia, Ikonge na Kiamogake kwenye eneobunge la Mugirango Kaskazini ni kati ya maeneo ambayo yametajwa, utata kuhusu kunakostahili kujengwa kwa chuo kikuu cha Nyamira ukiendelea kushamiri.

Kiabonyoru kwenye mpaka wa maeneobunge ya Borabu Kaskazini na Borabu pia imetajwa.

“Rais hajii eneo la Gusii kuzindua ujenzi wa Chuo Kikuu cha Nyamira. Anakuja kuanzisha ujenzi wa miradi mbalimbali hasa miundomsingi katika shule zilizopata ufadhili kutoka kwa serikali ya Kuwait,” akasema Bw Mogaka.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, Tume ya Elimu ya Juu (CUE) haijaamua eneo ambalo chuo hicho kitajengwa.

“Tulimweleza Rais kuwa baadhi ya miradi iliyozinduliwa haikuwa imeanza kutokana na ukosefu wa fedha. Tumemwambia asizindue ujenzi wa chuo kikuu kipya iwapo hakutakuwa na pesa za kuutekeleza ujenzi huo,” akasema Bw Mogaka.

Aliwataka wenyeji wasimakinikie uvumi unaoendelezwa na baadhi ya viongozi kuwa Rais anakuja Nyamira kuzindua ujenzi wa chuo kikuu.

Bw Nyamoko awali alikuwa amesema kuwa Rais Ruto atazindua ujenzi wa chuo hicho wakati wa ziara yake eneo la Gusii.

“Chuo Kikuu kitakuwa Kiabonyoru na mipango yote imekamilishwa huku Rais akitarajiwa kuzindua ujenzi wake,” akasema Bw Nyamoko wiki jana.

“Rais atazindua ujenzi wa mradi unaodhaminiwa na serikali ya Kuwait pale Kiabonyoru na kutangaza pia kuanzishwa kwa chuo hiki,” akaongeza Bw Nyamoko.

Rais Ruto alistahili kuanza ziara yake eneo la Gusii wiki jana lakini duru zinaarifu aliahirisha kutokana na viongozi wa eneo hilo kutokuwa tayari kuwa mwenyeji wake.

Pia, kuna madai eneo la Gusii linalalamika kutonufaika walivyotarajiwa baada ya baraza jipya la mawaziri kubuniwa kutokana na maandamano yaliyokuwa yakiendelezwa na Gen Z.

Kuhusu mahala pa ujenzi wa chuo kikuu, Bw Gisairo alimshutumu Bw Nyamoko akisema wanasiasa wa eneo hilo hawajakubaliana chuo hicho kijengwe Kiabonyoru.

“Tulikutana Mombasa na hatukuelewana kwa sababu kila moja alikuwa akitaka chuo hicho kijengwe eneo lake,” akasema Bw Gisairo.

Mbunge huyo alisema waliwaachia usimamizi wa Chuo Kikuu cha Kisii na CUE waamue eneo ambalo linastahili kwa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Nyamira.

Bw Gisairo aliongeza kuwa Nyamira ina kaunti ndogo tano na raslimali pamoja na ujenzi wa taasisi za masomo unastahili kufanyika kwa usawa.

Kaunti ya Nyamira haina chuo kikuu na mjadala wa ujenzi wa taasisi hiyo ya juu ya elimu ulianza wakati wa enzi za Gavana wa kwanza marehemu John Nyangarama.

Imetafsiriwa na Cecil Odongo