Habari za Kaunti

Wakulima wa miwa watishia kukataa kuipeleka viwandani

Na ANGELINE OCHIENG August 9th, 2024 1 min read

UZALISHAJI wa sukari nchini unaendelea kukabiliwa na changamoto huku wakulima wakiapa kusimamisha kwa muda uwasilishaji miwa kwa kampuni za sukari baada ya bei mpya kutolewa.

Hii inafuatia agizo la Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) la kutangaza bei mpya za miwa kuwa Sh4, 950 kwa tani kwa mwezi wa Agosti 7,2024.

Barua iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa AFA, Jude Chesire, ilisema kuwa hatua hiyo imetokana na kumalizika kwa muda wa kamati ya muda ya bei ya miwa na kutokuwepo kwa waziri wa kuteua kamati mpya wakati huo.

Baraza mpya la mawaziri liliapishwa jana.

Wakulima hao kupitia mwakilishi wao, Charles Atyang walisema wataacha kupeleka miwa kwa viwanda kuanzia Agosti 12 iwapo bei hizo mpya zitatekelezwa.

Bw Ayang alidai kuwa wakulima hawakushauriwa kabla ya kutolewa kwa bei hizo mpya.

“Barua hiyo ni lazima iondolewe mara moja, kamati ya kupanga bei ilikuwa imekubali kukagua bei na chochote tunachopata kama wakulima si sawa,” akasema Bw Atyang.

Mwakilishi huyo wa wakulima aliteta kuwa huku gharama ya uzalishaji ikiendelea kupanda, bei ya miwa imekuwa ikishuka.

Bei hizo mpya za miwa alisema zinawakatisha tamaa wakulima ambao wamewekeza katika uzalishaji huo wakiwa na matumaini ya kujikimu kimaisha.

Bw Ayang alisema kwa kuzingatia gharama ya sasa ya uzalishaji ya Sh6,500 kwa tani, wakulima hawapaswi kukubali bei yoyote iliyo chini ya hiyo.