Habari Mseto

Hasara panya wakivamia zao la mpunga Mwea

Na GEORGE MUNENE July 19th, 2024 1 min read

PANYA wamevamia mradi wa unyunyuzaji wa Mwea Kaunti ya Kirinyaga na kusababisha uharibifu mkubwa katika vitalu vya kukuzia mpunga.

Panya hao wanaharibu miche ya mpunga na wakulima wanaelezea hofu kuwa huenda wasipande msimu huu iwapo panya hao hawatadhibitiwa haraka.

“Tuna wasiwasi kuwa fuko hao huenda wakaangamiza miche katika vitalu ambavyo tumetayarisha,” mmoja wa wakulima, Bw Simon Njogu alisema.

Wakulima hao walisema panya hao huvamia vitalu hivyo nyakati za usiku na kuharibu miche hiyo ambayo baadhi iko tayari kupandwa.

“Tunatayarisha mashamba ya mpunga katika mradi ili tuweze kupanda lakini miche yetu mingi imeliwa na panya,” akaongeza Bw Njogu.

Wakulima hao walilalamika kwamba hata mitego iliyowekwa kwenye vitalu haisaidii.

“Panya ni wengi na hawawezi kudhibitiwa ipasavyo kwa kutumia mitego,” alisema Bw Njogu.

Wakulima hao walitoa wito kwa serikali ya kitaifa na kaunti kuingilia kati.

“Ni jukumu la serikali hizi mbili kuhakikisha kuwa miche yetu ya mpunga iko salama kwa utoshelevu wa chakula,” mkulima mwingine alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Kilimo na Seneta wa Kirinyaga, Bw Kamau Murango alikiri kuwa panya hao wameacha uharibifu katika mradi huo.

“Wakulima wanahesabu hasara na hatua za dharura zinafaa kuchukuliwa ili kuhakikisha kwamba miche haiharibiwi kabisa,” akasema Bw Murango.

Aliahidi kuomba serikali ya Kitaifa kudhibiti  fuko hao ambao ni tishio kwa wakulima.

Alisema wakulima wana mchango mkubwa katika uzalishaji wa mpunga na wanapaswa kusaidiwa.

Mradi huo, mkubwa zaidi nchini Kenya unachangia asilimia 80 ya mchele unaotumiwa kitaifa.