Habari za Kitaifa

Walimu wakataa uteuzi wa Waziri Ogamba


WALIMU katika Kaunti ya Kisumu wamekataa uteuzi wa Julius Migos Ogamba kama Waziri wa Elimu.

Walimu hao kupitia vyama vyao Jumatatu, Julai 22, 2024 walisema Bw Ogamba ambaye aliteuliwa na Rais William Ruto alipotangaza mawaziri 11 mnamo Ijumaa wiki jana, haelewi masuala ya elimu.

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Nchini (KNUT) tawi la Kisumu, David Obuon alisema waziri huyo mteule pia anaonekana haelewi msingi wa Mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC).

“Kwa sasa tunatekeleza mtaala wa umilisi na utendaji ambao unakabiliwa na changamoto tele, Bw Ogamba ni wakili kitaaluma na hatuelewi iwapo anafahamu masuala ya CBC,” akasema Bw Obuon.

“Wizara hii ina matarajio mengi ikiwemo kuwashirikisha washikadau nyanjani kuiendesha,” akaongeza.

Katibu wa Walimu Wakuu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai (KUPPET) tawi la Kisumu Zablon Awange, alisema kuwa sekta ya elimu Kenya inakabiliwa na changamoto tele ambazo zinahitaji kusuluhishwa kwa haraka.

Kati ya changamoto hizo ni bima ya afya, mkataba wa maelewano ya kuongeza walimu mshahara (CBA), wizi wa mitihani ya kitaifa, kupunguzwa kwa mgao wa serikali na sintofahamu kuhusu usimamizi wa sekondari za kiwango cha chini.

“Changamoto hizi zote zitatatuliwa tu iwapo mshikilizi wa wizara atakuwa mtu anayefahamu masuala ya elimu. Matatizo haya hayahitaji wakili ambaye alilemewa kutimiza ndoto yake ya kisiasa kama Bw Ogamba,” akasema Bw Awange.

“Tunaelewa uteuzi ni jukumu la Rais, ila kama viongozi lazima tumshauri,” akaongeza.

Mawaziri 11 walioteuliwa na Dkt Ruto, wanatarajiwa kupigwa msasa na Kamati ya Uteuzi Bunge la Kitaifa itakayoongozwa na Spika.

Endapo Bw Ogamba ataidhinishwa, atamrithi mtangulizi wake, Ezekiel Machogu.

Rais Ruto alivunja Baraza lake la Mawaziri baada ya shiniko la maandamano ya Gen Z.

Baadhi ya mawaziri waliohudumu katika baraza hilo, hata hivyo, waliteuliwa tena.