• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
AKILIMALI: Kijana alivyotumia teknolojia kuwazima mabroka wapunjaji

AKILIMALI: Kijana alivyotumia teknolojia kuwazima mabroka wapunjaji

NA FAUSTINE NGILA

FRANCIS Odoyo alijikuna kichwa kwa muda mrefu kila alipowaona wafanyabiashara wa nyanya kutoka kaunti za Siaya, Migori na Kisii wakisafiri hadi Kaunti ya Narok kununua bidhaa hiyo.

Alishangaa ni kwa nini nyanya haziwezi kukuzwa katika kaunti hizo. Baadaye aling’amua kuwa kaunti hizo hupata mvua nyingi ambayo huharibu zao hilo kwa kusababisha magonjwa, na wauzaji hulazimika kulinunua Narok ambako kuna jua kali.

Hapo ndipo wazo la kuwekeza kwenye kilimo hicho lilimjia. Lakini baada ya utafiti wa hapa na pale, aliamua kutumia teknolojia ya chumba cha mvugulio kufanikisha kilimo chake.

“Niliona kuna pengo kubwa katika soko la Migori. Niliamua kukukuza nyanya ndani ya mvugulio ili kudhibiti kiwango cha joto, kuzuia magonjwa  na kupunguza uharibifu,” anasema kijana huyu wa miaka 27.

Akiwa tayari amewahi kupunjwa na mawakala katika soko lake la nyumbani la Rongo, Kaunti ya Migori, aliamua kamwe hangewapa nafasi tena kuuza bidhaa zake kwa niaba yake.

“Mawakala hawa huishia kufaidika zaidi ya mkulima kwa kuwa hawapati gharama yoyote ya shambani, wao huishia kuwaumiza wakulima,” anasema kijana huyu ambaye pia anafanya kazi katika kampuni moja ya benki Narok.

Anasimulia kuwa kuna msimu alilazimika kuwauzia kreti moja kwa Sh1,800, ambazo ni hela ndogo sana. Walienda kuuza kila kreti kwa Sh5,4000.

“Nilifanya hivyo mara mbili kisha nikawakomesha. Wamezoea kuwapunja wakulima wa nyanya kwa kuwa wanajua zao hilo huharibika haraka,” anasema Bw Odoyo ambaye alihitimu shahada ya uanahabari katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara hapo 2013.

“Mawakala hawawezi kumruhusu mkulima kuuza moja kwa moja kwa wateja wa mboga. Ili kuwazima, niliwasaka kina mama wauzaji wa mboga nikazungumza nao na kuwashauri wawe wakija kununua kilo moja kwa Sh50 kutoka kwa shamba langu,” anasema.

Zao la nyanya lina faida mno. Anafichua kwamba katika chumba chake cha mvugulio alipanda mimea 1,000 ya nyanya. Kila mmea ulimzalia kilo 10 za nyanya na kuuza kila kilo kwa Sh50. Hivyo akatia mfukoni Sh500,000 za mauzo pekee.

Alitumia fedha alizohifadhi kutoka kwa kazi yake kuwekeza kwa chumba cha kwanza cha mvugulio, mabomba ya kunyunyizia maji, tanki la maji la lita 1,000, mbegu za nyanya na huduma za wataalamu wa mchanga, zote  kwa gharama ya Sh220,000.

Kutokana na mauzo tangu aanzishe mradi huo hapo Januari 2016, kwa sasa ameweza kupanua kilimo chake na kumiliki vyumba viwili vya mvugulio.

Francis Odoro akikagua mimea yake ya nyanya katika chumba cha mvugulio eneo la Rongo, Kaunti ya Migori. Picha/ Faustine Ngila

Amepanda nyanya kwa mitaro laini ndani ya mvugulio huku mabomba yakipangwa vyema ndani ya mchanga ili maji yafikie mizizi ya mimea.

“Hapa maji sio tatizo, tumechimba kisima. Ninachohitaji ni pampu ya kupiga maji hayo hadi kwa mimea,” anasema Bw Odoyo ambaye amemwajiri mfanyakazi mmoja kumsaidia kwa shughuli za shambani wakati akiwa mbali.

Aidha anawaonya wakulima ibuka wa nyanya kuwa ni makosa sana kupuuza mchanga kupimwa kuhusu magonjwa na kiwango cha asidi, kabla ya kupanda miche.

Anasema yeye mwenyewe amejifunza hilo baada ya mimea yake kuvamiwa na ugonjwa wa kunyausha majani, pindi tu iliponza kuota maua, na kumsababishia hasara katika mojawapo ya misimu.

“Ingawa kupimiwa mchanga kuna gharama zake, usiogope hiyo gharama kwa kuwa haiwezi kufikia hasara utakayopata ukikosa kupimiwa mchanga na kuubadilisha iwapo una magonjwa,” anashauri.

Hata hivyo, yeye alijaribu kung’oa mimea iliyoambukizana ugonjwa huo, na hatimaye kupulizia dawa, lakini tayari hasara ilikuwa ishaingia.

Bw Dennis Ongech, ambaye ni mtaalamu wa mimea katika shirika la Hortitechno Produce anasema kuwa ugonjwa wa bakteria wa majani kunyauka ni tisho kuu kwa wakulima kutoka magharibi mwa nchi.

“Wakati unaona ncha ya mimea yako ikijikunja wakati kuna maji ya kutosha, jua kwamba ugonjwa huo umeanza kuvamia mimea. Ing’oe mara moja mimea iliyoathiriwa,” anashauri mtaalamu huyo.

Bw Odoyo anasema kuwa wakati mwingine yeye husitisha upanzi wa nyanya kwanza, ili kuupa muda udongo kurejea kwa hali ya awali, kwa kupanda mmea mwingine.

“Upo msimu niliepuka kupanda nyanya nikapanda spinachi ili angalau kupunguza kiwango cha asidi mchangani maanake ninatumia fatalaiza kwa kilimo changu. Msimu uliofuata nilivuna vizuri kutokana na nyanya,” anasema Bw Odoyo.

Huku akiwalaani mawakala walaghai, anaishangaa serikali kuzembea katika kuweka sheria ya kuwafungia nje maajenti wanaowapunja wakulima wenye bidii kila uchao.

Mtafiti wa sera za kilimo katia Chuo Kikuu cha Egerton Haggai Oduori anawashauri wakulima kujiunga kwa mashirika ya kilimo ili kujikinga dhidi ya mabroka, kwa kuwa serikali inajikokota kuwalinda wakuzaji mimea.

You can share this post!

Mutuma Mathiu ateuliwa Mkurugenzi Mhariri mpya NMG

Heroini: DPP ataka mshukiwa aozee jela miaka miaka 22

adminleo