Habari za Kitaifa

Ujio wa wandani wa Raila serikalini wagawa Mulembe Natembeya akivumisha wimbi la ‘Tawe’

Na SHABAN MAKOKHA July 31st, 2024 2 min read

MGAWANYIKO mkubwa umezuka kati ya viongozi wa jamii ya Mulembe kuhusu hatua ya Rais William Ruto kuwajumuisha baadhi ya viongozi wa ODM ndani ya serikalini.

Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya ameongoza mrengo wa wanasiasa kutoka Magharibi kutaka utawala wa Kenya Kwanza utekeleze ahadi ya kutoa asilimia 30 za nyadhifa kwa wakazi wa eneo jinsi ilivyosema wakati wa kampeni za 2022.

Bw Natembeya amesema ni wazi kuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi, wameshindwa kutoa uongozi bora kwa wakazi wa eneo hilo na sasa ni wakati wa kupisha uongozi mpya.

“Tunataka kujua jinsi eneo hili linanufaika kisiasa chini ya Wetang’ula na Mudavadi. Tunataka watuambie miradi ambayo wameanzisha au ile ambayo imetekelezwa tangu waingie mamlakani,” akasema Bw Natembeya.

Gavana huyo ambaye ameanzisha vuguvugu la tawe ameanza kuwavutia Katibu wa UDA Cleophas Malala, mfanyabiashara nguli wa Kakamega Cleophas Shimanyula ‘Toto’ na waziri wa zamani wa michezo Rashid Echesa katika mrengo anaouongoza.

“Mudavadi na Wetang’ula wote wanadai kuwa wana nyadhifa kuu serikalini ilhali viwango vya umaskini Magharibi vinaendelea kupanda. Sasa ni dhahiri wawili hao wanashughulikia maslahi yao wala si ya wananchi,” akaongeza.

Wanasiasa hao wanasema wakati umefika ambapo Mabw Mudavadi, Wetang’ula na waziri mteule wa vyama vya ushirika na biashara ndogondogo Wycliffe Oparanya kuwapisha wanasiasa chipukizi.

“Sasa kwa sababu mirengo yote ya Mulembe ipo serikali, tunataka kufahamu jinsi ambavyo watu wetu watanufaika,” akasema Bw Malala ambaye pia alikuwa katika mkutano huo ambao ulifanyika mjini Kakamega wikendi.

Bw Echesa naye ametofautiana na Rais Ruto akisema kuwa amewasaliti watu ambao walihakikisha anapata kura za maana Magharibi wakati ambapo ilikuwa vigumu kuvumisha UDA eneo hilo.

“Nilipewa wadhifa ambao nalipwa Sh50,000 kila mwezi na Sh54,000 kwa kila kikao tunachoandaa japo vikao hivyo havizidi nne kwa mwaka. Hili ni jambo la kuchekesha,” akasema Bw Echesa.

Hata hivyo, viongozi ambao wanaunga mkono ushirikiano kati ya Raila Odinga na Rais William Ruto wamesema kuwa wanaunga mkono uteuzi wa Bw Oparanya kama waziri.

Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula na Mbunge wa Mumias Masharki Peter Salasya walisema kuwa Mabw Mudavadi na Wetang’ula ndio wataongoza mkutano wa kusherehekea uteuzi wa Bw Oparanya.

Bw Savula alidai kuwa Bw Natembeya anadhaminiwa na baadhi ya wanasiasa wakuu serikalini ili kuwadhalilisha Mabw Mudavadi na Wetang’ula na kusambaratisha umoja wa Waluhya.

“Tunawajua na wale ambao wanawadhamini na hawataenda mbali. Nimekuwa mbunge na sasa naibu gavana na najua Malala, Echesa na Natembeya hawaendi popote. Wangemakinikia kujijenga kisiasa badala ya kutumiwa kuwapiga vita Waluhya,” akasema Bw Savula.