Habari za Kitaifa

Knut yataka usalama uimarishwe maeneo yanayokumbwa na ujangili kabla ya mitihani kuanza

Na VITALIS KIMUTAI September 23rd, 2024 1 min read

CHAMA cha Kitaifa cha Walimu nchini (KNUT) kinaitaka serikali kushughulikia kikamilifu masuala ya ukosefu wa usalama katika maeneo yanayokumbwa na ujangili kabla ya mitihani ya kitaifa kuanza.

Bw Malel Langat, Makamu Mwenyekiti wa Kwanza wa Kitaifa wa chama hicho alisema kuna wasiwasi mkubwa miongoni mwa wadau wa elimu kwamba idadi kubwa ya shule haziwezi kufikiwa na wanafunzi na walimu mwezi mmoja baada ya taasisi hizo kufunguliwa kwa muhula wa tatu.

Haya yanajiri huku Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) likijiandaa kwa mitihani ya Elimu ya Shule za Msingi (KPSEA) na kidato cha nne (KCSE) kote nchini.

“Maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni Pwani, Kaskazini mwa Bonde la Ufa na Kaskazini Mashariki mwa Kenya ambako kwa bahati mbaya viwango vya juu vya ukosefu wa usalama vimewafukuza walimu na wanafunzi shuleni. Hili ni suala ambalo serikali inapaswa kushughulikia kwa haraka na kurejesha utulivu,” Bw Langat alisema.

Bw Langat alisema inasikitisha kwamba ingawa masomo yanaendelea kama kawaida katika shule nyingi nchini, kuna shule ambazo hazifikiki ilhali watoto watafanya mitihani sawa na wengine ambao hawajaathiriwa.

“Ujangili na ukiukaji wa sheria katika maeneo nchini Kenya umefanya watu kupoteza maisha,  kuhama makwao na kufungwa kwa shule hasa Lamu, Tana River, Turkana, Baringo, Samburu, Laikipia, Mandera, Garissa, Wajir, Elgeyo Marakwet. , Pokot Magharibi miongoni mwa maeneo mengine tete,” Bw Langat alisema