MAONI: Rais apuuze ushauri wa watu kama Atwoli
IKIWA kuna mtu ambaye Rais William Ruto na Wakenya wanaowazia mema nchi hii wanafaa kujihadhari naye, ni Bw Francis Atwoli, Katibu Mkuu mkongwe wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU).
Bw Atwoli ni mwepesi wa kuropokwa wakati mwingine bila kupima athari za kauli zake kwa mustakabali wa nchi hii.
Mmoja wa ushauri ambao alimpa Rais Ruto mnamo Jumapili ni wa kubadilisha katiba ili kunyima Wakenya haki yao ya kwenda kortini kulalamikia ajenda na mipango ya serikali wanayohisi inawakandamiza.
Kwa ufupi, kile ambacho Bw Atwoli anamshauri Rais Ruto kufanya ni kuhakikisha kwamba hakuna Mkenya anayepaswa kuuliza swali lolote kuhusu miradi ya serikali ikiwemo inayotumiwa kupora pesa za umma ilivyothibitishwa na ripoti kadhaa za kamati za Bunge la Kitaifa, Mkaguzi Mkuu wa Serikali na Mdhibiti wa Bajeti.
Inasikitisha Bw Atwoli ambaye amekuwa katika nchi hii kwa miaka mingi na anayejigamba kuwa mwanachama wa Kanu, chama kilichovuruga katiba ya zamani kutimiza maslahi ya waliokuwa mamlakani wakisingizia walilenga kunufaisha raia anataka kurudisha nchi enzi kama hizo za giza.
Nadhani Rais Ruto hajasahau msimamo na kauli za Bw Atwoli alipokuwa akimpinga wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022 hasa tamko maarufu la “kateni miti”.
Itakuwa balaa kuanzisha mageuzi ya kikatiba kwa lengo la kuzuia raia kusaka haki mahakamani wakati ambao wawakilishi wao katika Bunge la Kitaifa wamekengeuka.
Ushauri wa Atwoli kwa Rais Ruto unaenda kinyume na kiapo cha afisi kuu ya kiomgozi wa nchi cha kulinda na kutetea Katiba.
Alichofanya Atwoli ni kumtaka Rais kurarua katiba yenyewe huku akisahau uamuzi wa Mahakama ya Juu katika kesi za uliokuwa Mpango wa Maridhiano (BBI) kwamba rais hawezi kuanzisha mchakato wa kubadilisha katiba.
Huu wa Atwoli, ashakum sio matusi, ni ushenzi.