Habari

Kilio polisi wakihangaisha wamiliki wa baa kwa kutowapa hongo

Na STANLEY NGOTHO January 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAMILIKI wa baa na mikahawa mjini Kitengela wanalalamika kwamba wananyanyaswa na maafisa wa polisi hatua inayoweza kuwafanya wafunge biashara zao.

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, kurasa za mitandao tofauti ya kijamii katika mji huo wenye watu wengi imekuwa ikijaa shutuma zinazowalenga afisa wa polisi fisadi na wasaidizi wake katika kituo cha polisi cha Kitengela.

Hongo hizo zinazodaiwa kupewa jina la ‘malipo ya ulinzi’ zinasemekana kuwa kati ya Sh5,000 kwa baa ndogo na Sh 10,000 kwa baa kubwa kila mwezi.

Madai hayo yalifanya Taifa Leo kuchukua hatua siku ya Jumatatu kukutana na waathiriwa kadhaa wa unyanyasaji huo katika mji wa Kitengela.

Katika baa na mkahawa ambao mmiliki ana leseni katika eneo la Kyang’ombe ndani ya mji wa Kitengela, Bi Jacinta* aliketi kwenye kiti cha plastiki nje ya biashara yake akiwa na mawazo tele.

Aliambia Taifa Leo kwamba biashara yake ilivamiwa na maafisa wa polisi mwishoni mwa juma na wakachukua vileo vyote vya thamani ya maelfu kwa kuchelewa kulipa ada ya ulinzi ya Sh5,000.

“Nilitakiwa kutoa hongo ya Sh5,000 siku ya Ijumaa lakini nilikosa kutokana na matatizo ya kifedha ya biashara,” alisema.

“Maafisa hao walivamia biashara yangu na kubeba pombe yote kama ushahidi wa mashtaka ya uongo ikiwa ni pamoja na kuhudumu baadai muda unaohitajika,” Anamshtumu afisa wa kituo cha polisi cha Kitengela anayehusika na uhalifu kwa kudai Sh 15,000 ili kuachilia pombe hiyo la sivyo ashtakiwe mahakamani.

Taifa Leo imebaini kuwa ofisi ya makosa madogo inaongozwa na Inspekta wa Polisi Zacchaeus Anindo. Mmiliki mwingine anayehudumu mtaa wa EPZ alisema aliangukia kwenye mtego huo na alilazimika kulipa Sh30,000 kutoka Sh50,000 alizoitishwa na afisa wa cheo cha Inspekta wa polisi baada ya mazungumzo ya muda mrefu.

“Kituo cha polisi cha Kitengela kimeoza kabisa. Baa na mikahawa imekuwa ng’ombe wa maafisa tapeli kukama pesa. Wamiliki wa baa ambao hawalipi wanakabiliwa na ghadhabu ya mafiasa hao” aliambia Taifa Leo akisema anafikiria kuhama au kufunga biashara hiyo.

Mmiliki mwingine wa baa kando ya barabara ya Miriam aliambia Taifa Leo kwamba ni baa pekee zinazomilikiwa na maafisa wa polisi ndizo zinazoepushwa unyanyasaji huo.

“Maafisa wana orodha ya baa zote mjini na tarehe wanazotakiwa kukusanya ada za ulinzi. Ni baa tu zinazomilikiwa na wenzao ndizo zinazoepukwa. Pindi mwenye baa analipia ulinzi, anaruhusiwa kufanya kazi kwa saa 24,” aliambia Taifa Leo na kuomba asitajwe jina asidhulumiwe zaidi.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Baa na Mikahawa katika Kaunti ya Kajiado Stanley Njuguna aliambia Taifa Leo kwamba suala hilo hapo awali liliripotiwa kwa kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Isinya mara tatu lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.

“Unyanyasaji huo unalenga wanachama wetu na wale ambao hawajasajiliwa. Tuna matukio ambapo maafisa wa uhalifu wadogo wanawadhulumu watu wanaokataa kutoa rushwa inayoitwa ada za ulinzi,” aliongeza.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Isinya Patrick Manyasi alikanusha kufahamu madai hayo akiwataka waathiriwa kuripoti kisa chochiote kama hicho katika kituo cha polisi.

“Sijafahamishwa kuhusu tuhuma hizo nzito. Acha mwathirika apige ripoti rasmi katika kituo cha polisi. Ninaweza tu kuchukua hatua ikiwa suala hilo limefikishwa kwangu na OCS. Kuna mifumo ya Huduma ya Polisi ya kuwaadhibu maafisa wanaokika sheria,” akasema Bw Manyasi.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA