Jamvi La Siasa

Rais aegemea kwa mawaziri kumpigia debe kura za 2027

Na JUSTUS OCHIENG, BENSON MATHEKA April 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto ameanza harakati za mapema kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027, akionekana kutegemea mawaziri wanasiasa kumpigia debe huku akikabiliwa na changamoto tele.

Mawaziri hawa, wakiwemo wa chama cha ODM chini ya Serikali Jumuishi, sasa wamechukua nafasi muhimu katika siasa za kitaifa, wakiongoza mikutano ya hadhara, vikao vya mashauriano na hata ziara za kukagua miradi ambazo zinatumika kama jukwaa la kuuza ajenda ya Kenya Kwanza na kumpigia debe Rais Ruto.

Kabla ya ziara zake za hivi karibuni maeneo ya Mlima Kenya, Rais Ruto alifanya mikutano ya faragha na viongozi wa kisiasa na wa serikali kutoka eneo hilo akiwemo Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, mawaziri, makatibu na viongozi wa nyanjani ili kuratibu ujumbe wa kuhakikisha alionekana kuungwa mkono.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa Rais ana muda wa kutosha kujipanga upya na kurekebisha makosa, lakini pia anakabiliwa na changamoto kubwa kama vile mgawanyiko wa ndani, matatizo ya kiuchumi, hasira za vijana na upinzani unaojipanga upya.

Katika kukabiliana na hali hiyo, mawaziri wanasiasa wamechukua jukumu la kumtetea na kumvumisha Rais Ruto kwa bidii, wakiahidi maendeleo na kushambulia upinzani.Zaidi ya nusu ya mawaziri wake ni wanasiasa ambao wana ushawishi katika maeneo mbalimbali wanakotoka.Miongoni mwa mawaziri walio mstari wa mbele ni pamoja na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye pia anaongoza wizara ya masuala ya nje.

Katika hatua ya kushangaza, Bw Mudavadi alikubali kuunganisha chama chake cha Amani National Congress (ANC) na UDA cha Rais Ruto, akisema ni hatua ya kuimarisha muungano wa Kenya Kwanza na kuleta utulivu wa kisiasa kuelekea 2027.“Muungano huu si wa maslahi ya kibinafsi bali wa kutimiza ahadi tulizotoa kwa wananchi,’ alisema Bw Mudavadi katika taarifa ya hivi majuzi.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen azungumza na wanahabari katika jumba la Harambee, Nairobi akiandamana na makatibu katika wizara hiyo Salome Muhia (kushoto) na Raymond Omollo hivi majuzi. PICHA|MAKTABA

Waziri wa Usalama wa Ndani, Bw Kipchumba Murkomen pia amekuwa mstari wa mbele kumtetea Rais Ruto katika mikutano mbalimbali ya hadhara na mazishini wanavyofanya wenzake ambao ni wanasiasa.

Alilinganisha hali ya sasa ya kisiasa na ile ya mwaka 2005 ambapo Rais wa wakati huo Mwai Kibaki, alikumbwa na upinzani mkubwa baada ya kupoteza kura ya maamuzi lakini baadaye, alishinda muhula wa pili chini ya chama cha PNU.

“Changamoto zinazomkumba Rais Ruto si mpya. Tuliziona kwa Kibaki mwaka 2005. Alidhaniwa amemalizwa kisiasa lakini aligeuka kuwa mmoja wa marais wanaosifiwa zaidi,”alisema Bw Murkomen.Waziri huyo alisema kuwa hatua ya Ruto kuunda serikali jumuishi ni njia bora ya kuunganisha taifa na kuleta utulivu, akiwapuuza wanaobeza serikali ya sasa.

Waziri wa Ardhi Alice Wahome amefichua kuwa amekuwa akilengwa na kambi ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ili kujiondoa serikalini, lakini ameapa kubaki ndani ya serikali kwa kuwa anamuunga mkono Profesa Kindiki ambaye ‘ni mwana wetu’ kutoka eneo la Kati.“Walitushawishi kuondoka lakini hatuondoki. Serikali hii ni yetu, na tumejizatiti kuitetea hadi mwisho,” alisema Bi Wahome.

Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini Hassan Joho.

Mawaziri kutoka maeneo mengine kama vile Hassan Joho (Madini), John Mbadi (Hazina), Opiyo Wandayi (Nishati) na William Kabogo (ICT) pia wamekuwa wakimpigia debe Rais waziwazi.

Mawaziri wengine wanasiasa ni Wycliffe Oparanya( Ushirika) Alfred Mutua( Leba), Aden Duale( Afya) Soipan Tuya( Ulinzi) na Salim Mvurya ( Michezo)Mabw Mbadi na Wandayi wamekosolewa na baadhi ya wanasiasa wa upinzani kwa kujiunga na kwaya ya kusifu Rais Ruto lakini wanasema kuwa wako kazini na ni haki yao kuunga mkono ajenda ya serikali.

Wandani wa Raila ambao ni mawaziri

Bw Joho, kwa upande wake, amekuwa mshambuliaji mkubwa wa wakosoaji wa serikali wanaotumia mitandao ya kijamii. “Waendelee kupiga kelele mtandaoni, sisi tuko mashinani tukifanya kazi,” alisema Bw Joho akiwa Mombasa.Rais Ruto ameonekana kujifunza kutoka kwa makosa ya awamu ya kwanza ya uongozi wake pamoja na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ambapo baadhi ya mawaziri walionekana kuwa mbali na wananchi.

Kwa kuwaweka mawaziri wake mstari wa mbele kumpigia debe mapema, Rais Ruto analenga kuimarisha ushawishi wa kisiasa na kukabiliana na changamoto kutoka kwa wapinzani.