Akili MaliMakala

Mafuta ya ngamia yanavyobadilisha maisha ya wafugaji

Na SAMMY WAWERU September 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

GARISSA Butchers Saving and Cooperative Society, ni chama cha ushirika cha wafugaji kutoka eneo la Kaskazini Magharibi mwa Kenya ambacho kimeletea wanachama wake mageuzi makubwa kimaendeleo. 

Ukiwa ulianzishwa 2021, ni muungano unaoleta pamoja wafugaji wa ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo, lengo likiwa kuwasaidia kupata masoko yenye ushindani mkuu.

Ngamia, ameibuka kuwa mnyama mwenye tija chungu nzima, kando na kuuza nyama zake na maziwa, chama hicho sasa kikiteka soko jingine – mafuta.

Wanaunda mafuta ya kupika na kujipodoa, kutokana na nyama za mifugo hao ambao kwa wakazi wa Kaskazini Mashariki ni dhahabu.

Mafuta ya ngamia yliyoundwa na wanachama wa Garissa Butchers Saving and Cooperative Society

Kabla ya kuasisiwa, walitegemea kuuza nyama za ngamia kila siku, na zinapokosa kununuliwa kuisha, walikuwa wakipata hasara kwa sababu ya kukosa miundombinu faafu kuzihifadhi, kama vile jokofu.

“Kukosa kuuza nyama zote kwa siku, ni hasara kubwa kwa mfugaji,” anasema Naibu Mwenyekiti Garissa Butchers Saving and Cooperative Society, Abdi Bulle.

Leo hii, kupitia ushirika huo, wanachakata nyama na mifupa ya ngamia kuzalisha mafuta yenye thamani kubwa.

Aidha, hutoa mafuta kwenye mifupa na nundu. Chama hicho kupitia kichinjio chake huchinja wastani wa ngamia 35 kwa siku, wakikadiria kuzalisha karibu lita 25 za mafuta.

“Siku nzuri, tunatoa hadi lita 10 za mafuta ya mifupa (bone marrow oil) na lita 15 kutoka kwenye nundu (hump oil),” Abdi anafafanua.

Naibu Mwenyekiti Garissa Butchers Saving and Cooperative Society, Abdi Bulle (kulia), anasema ukamuaji wa mafuta kutoka kwa nguruwe ni biashara inayoingizia wafugaji wa Garissa pesa. Pesa|Sammy Waweru

“Hata ingawa wafugaji kitambo walikuwa wakizalisha mafuta ya ngamia, kupata soko ilikuwa kibarua. Muungano umewasaidia kupenyeza bidhaa zao sokoni, kupitia mikakati iliyowekwa ikiwa ni pamoja na kunogesha mauzo.”

Ikilinganishwa na hapo awali, bei imeimarika. Lita moja ya mafuta ya bone marrow huuza Sh2, 500, huku mafuta ya nundu yakiwa Sh1, 700 kwa lita.

Hali kadhalika, kilo moja ya nyama za ngamia kupitia chama hicho wafugaji wanalipwa Sh1, 000, ikilinganishwa na Sh500 hapo awali. Wanachama wanakiri maisha yao kubadilika kimaendeleo.

“Kabla ya kujiunga, nilikuwa nikiunda mafuta nyumbani lakini kupata soko haikuwa rahisi. Nyakati zingine nilikuwa nikikaa hadi majuma matatu bila kupata mnunuzi. Kwa sasa, bidhaa zangu zikiwa tayari zinauzwa kupitia chama cha ushirika,” anasema Mama Asha Abikar.

Anasema, sasa imekuwa rahisi kulea wanawe muungano huo ukiwaletea faraja. Mbali na mafuta, ushirika huo pia hutoa mikopo isiyo na riba kwa wanachama wake.

Baadhi ya kina mama wanachama wa Garissa Butchers Saving and Cooperative Society wakati wa hafla ya Kenya Meat Expo & Conference 2025, Nairobi. Picha|Sammy Waweru

Mfanyabiashara Yussuf Sigat anaeleza: “Kuna wakati buchari yangu ilikuwa karibu kuanguka. Nilipata mkopo wa Sh100, 000 bila riba, na sasa biashara yangu imeboreka.”

Mikopo, inatokana na hela ambazo wanachama hutoa kila mwezi. Abdi, anafichua kwamba kwa mfugaji kuwa memba lazima atoe ada ya Sh500 za kujiandikisha na kila mwezi mchango wa Sh1, 000.

“Pesa hizo ndizo huwakopesha wajiimarishe, pamoja na biashara zao,” anaelezea.  Ni mafanikio makubwa, anayosema yalitokana na wazo la waanzilishi wawili – kama wakurugenzi wakuu, janga la Covid lilipotua nchini 2020.

Miaka minne baada ya chama hicho kuanzishwa rasmi, sasa kinajivunia kuwa na wanachama 60. Kaskazini Mashariki mwa Kenya, inaorodheshwa kama eneo kame (ASAL), na Abdi anasema athari za tabianchi zimechochea ngamia kupungua.

Mafuta ya ngamia na nyama zilizoongezwa thamani – nyirnyir na Garissa Butchers Saving and Cooperative Society. Picha|Sammy Waweru

“Tumelazimika kupunguza idadi ya wanaochinjwa kutoka 50 hadi 35 kwa siku kwa sababu ya ukame,” Abdi anasema. Licha ya changamoto hiyo, soko la mafuta ya ngamia linaendelea kukua, huku jamii zingine zikianza kuyakumbatia.

Kupitia msaada wa mashirika kama Mercy Corps na serikali ya kaunti, Garissa Butchers Saving and Cooperative Society sasa ina mitambo ya kisasa ya kuunda bidhaa kama sausage na nyirinyiri – nyama za ngamia zilizokaushwa, zikapikwa na kupakiwa. Umoja ni nguvu, Abdi anasisitiza, akiongeza kuwa ushirikiano na ubunifu ndio siri ya mafanikio ya wafugaji kutoka Garissa.