Haki msiniaibishe nikose tiketi, Kalonzo alilia ngome yake
KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amesema ndoto yake ya kugombea urais mwaka wa 2027 inaweza kuyeyuka endapo mgombea wake atashindwa katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Mumbuni Kaskazini, Kaunti ya Machakos.
Bw Musyoka alisema wapinzani wake wa kisiasa, akiwemo Naibu Rais Rigathi Gachagua, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya na aliyekuwa waziri Fred Matiang’i, watamtania iwapo chama chake kitapoteza kiti hicho kidogo cha uwakilishi.
“Wakinitania watasema, ‘Kalonzo anataka kuwa rais wa Kenya na hawezi kushinda hata kiti cha wadi’. Nisaidieni kuepuka aibu hii. Wamenitegea mtego — nisaidieni kuuruka,” alisema Bw Musyoka Jumanne wakati wa mahafali ya kwanza ya Machakos Youth Service mjini Machakos.
Kiongozi huyo wa Ukambani alitumia fursa hiyo kuwataka wakazi kumpigia kura Antony Kisoi, mgombea wa Wiper katika uchaguzi huo mdogo, akisema ushindi wake utakuwa ishara ya nguvu za chama hicho na utiifu wa jamii ya Wakamba.
Seneta wa Machakos Agnes Kavindu na Naibu Gavana Francis Mwangangi pia wameeleza kuwa uchaguzi huo mdogo ni “kipimo cha mapema” kwa kinyang’anyiro cha urais mwaka wa 2027.
“Ushindi wa Bw Kisoi utathibitisha kwamba Kalonzo ndiye anayestahili kuwa mgombea urais wa upinzani kwa sababu anaheshimika si tu Ukambani bali nchini kote,” alisema Bi Kavindu katika mkutano wa hadhara hivi majuzi.
Bw Mwangangi aliongeza kuwa uchaguzi huo mdogo unapaswa kuwa “funzo kwa Rais Ruto”, akisisitiza kuwa ni fursa ya kudumisha shinikizo la vijana dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza.
Kampeni hizo zimeibua mvutano miongoni mwa wandani wa Rais Ruto Ukambani baada ya vyama vya UDA na Maendeleo Chap Chap (MCC) kuweka wagombea tofauti.
UDA imemteua mfanyabiashara Misi Mutua, huku MCC, kinachohusishwa na Waziri wa Kazi na Ulinzi wa Jamii Dkt Alfred Mutua, kikimpendekeza Harrison Wambua.
Wawili hao wanatoka maeneo tofauti ya wadi hiyo, huku Bw Mutua akiwa na ngome kubwa katika eneo la Mung’ala lenye wapiga kura wengi. Wachanganuzi wa kisiasa wanasema ushawishi wa chama ndio utakaobainisha mshindi wa kiti hicho.
Chama cha Maendeleo Chap Chap kinasema kina haki ya kuhifadhi kiti hicho kwa kuwa aliyekuwa MCA marehemu Gideon Kavuu alichaguliwa kupitia chama hicho mwaka wa 2022.
Kampeni za wagombea hao wawili zimeathiriwa na ushindani wa kindugu kati ya Dkt Mutua na Mbunge wa Mwala Vincent Kawaya, ambaye amekuwa akimtaka Dkt Mutua “kuvunja chama cha Maendeleo Chap Chap na kujiunga na UDA” endapo anaunga mkono Rais Ruto kwa dhati.
Kwa upande wake, chama cha Wiper kinatarajia kutumia migawanyiko hiyo kujidhihirisha ushawishi wake Ukambani kupitia ushindi wa Bw Kisoi.
“Tumuunge mkono Bw Kisoi kwa sababu ushindi wake si wake binafsi — ni ushindi wa chama chetu, kiongozi wetu Kalonzo Musyoka, na fahari kwa jamii nzima ya Wakamba,” alisema Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti.