Habari

Shinikizo zaidi TZ iachilie miili ya waliouawa wakati wa maandamano

Na CHARLES WASONGA December 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUNDI la mataifa 14 ya Bara Uropa yameitaka serikali ya Tanzania kuachilia miili ya watu waliouawa katika ghasia za wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, mwaka huu.

Kwenye taarifa Ijumaa Desemba 5, 2025 mataifa hayo pia yameitaka serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa na kutoa huduma za kimatibabu na kiafya kwa watu wengine wanaozuiliwa kwa tuhuma za kuhusika na fujo hizo.

Mataifa hayo ni pamoja na Uingereza, Ujerumani, Canada, Ufaransa, Italia, Uholanzi, Poland, Slovakia, Uhispania, Uswidi, Denmark, Norway na Umoja wa Ulaya (EU).

“Tunaitaka serikali ya Tanzania kuchukua hatua ya haraka na iachilie miili yote ya waliouawa ili wakachukuliwe na familia zao na iwaachilie huru wafungwa wa kisiasa,” ikasema taarifa hiyo iliyotiwa saini na mabalozi wa mataifa hayo.

Mnamo Novemba 12, 2025, Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi alithibitisha kuwa maiti ya Mkenya John Ogutu, mwalimu katika Shule ya Sky Schools iliyoko Dar es Salama, aliyeuawa kwa kupigwa risa Oktoba 29 haukuwa umepatikana.

“Wizara inaelezea hofu kuwa mwili wa Ogutu haijapatikana hadi sasa,” akasema

Akaongoza: Tunafanya mazungumzo ya serikali ya Tanzania ili tusaidiwe kupata mwili wa Ogutu na kuachiliwa huru kwa Wakenya wengine watatu wanaozuiliwa korokoroni.”

Kulingana na taarifa ya mabalozi hao wa mataifa ya Uropa chunguzi zilizoendeshwa na mashirika ya kutetea ya Tanzania na ya kimataifa yametoa ripoti kuonyesha visa vya mauaji ya kiholela watu kutoweka, wengine kukamatwa na maiti kufichwa wakati wa ghasia hizo.

Mabalozi hao walimtaka Rais Suluhu kutekeleza mapendekezo yaliyolewa na Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Afrika Kusini (SADC) kwenye ripoti yake ya kwanza kuhusu jinsi uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 ulivyoendeshwa.

Kwenye ripoti zake, AU na SADC zilitambua mapungufu katika mchakato wa uendeshaji uchaguzi na dosari nyinginezo kama vile kuteketezwa kwa karatasi na vifaa vya uchaguzi hali iliyoitilia shaka uhalali wa matokeo haswa wa uchaguzi wa urais.

Mabalozi hao wa mataifa ya kigeni pia walishinikiza kufanyike uchunguzi huru, yenye uwazi na unaoshirikisha wote, kuhusu ghasia hizo za uchaguzi nchini Tanzania.

Aidha, waliitaka serikali ya Tanzania kuwajibika kwa kulinda haki za kikatiba, haswa ya kupata habari na uhuru wa kujieleza miongoni mwa raia wa Tanzania.

Wito wa mataifa hayo ya bara Uropa umejiru siku moja baada ya Amerika kutangaza kuwa utafanya mabadiliko makubwa kuhusu uhusiano kati yake na Tazania kutokana na mauaji ya wakati na baada ya uchaguzi mkuu.